Ditopile ampongeza Rais Samia kwa kumtua mama kuni kichwani



Na Mwandishi Wetu


MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Mariam Ditopile amegawa mitungi 250 ya gesi safi ya kupikia kwa viongozi wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania ( UWT) Wilaya ya Kondoa, lengo likiwa kutekeleza mpango wa taifa wa kumtua mama kuni kichwani.


Ugawaji huo wa mitungi ya gesi iliyoungwanishwa na jiko la kupikia umefanyika leo Oktoba 13, 2023 wilayani Kondoa, wakati akizungumza na wanawake wa UWT ambao wanaadhimisha wiki ya UWT katika Wilaya hiyo.


Uamuzi huo wa kugawa mitungi hiyo ni kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuondoa nishati chafu ya kupikia kama kuni na mkaa na kuhimiza jamii itumie nishati mbadala.


"Leo tuko hapa katika maadhimisho ya UWT Wilaya ya Kondoa na kila mwaka huwa tufanya wiki ya UWT kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa mpaka Taifa.


Akifafanua zaidi anasema katika kuadhimisha Wiki ya UWT ameona ni vema akafanya jambo ambalo limeasisiwa na Rais wetu  Dk.Samia Suluhu Hassan  mwaka 2022  kupitia Wizara ya Nishati ambapo kulifanyika kongamano la kuhamasisha 

nishati safi ya kupikia.


"Tunataka  kumkomboa mwanamke lakini kuni zinaua sana mama zetu , kuni zinaleta matatizo makubwa kwa mama zetu,  Serikali yetu kupitia Rais Samia ameendelea kutafuta nishati safi ya kupikia. Akiwa Makamu wa Rais alipambana na kumtua ndoo mama kichwani na leo tunaona matunda yake, " amesema.


Amewaeleza wanawake hao wa UWT kwamba mitungi hiyo ambayo ameigawa leo inatokana na fedha za Samia Suluhu Hassan ambaye ni jasiri muongozaa njia kwani  kupitia Bunge alileta bajeti ya ruzuku ya kununua mitungi ya gesi na asigawe yeye ipite kwa wabunge.


"Sisi ni nani tusirudishe sifa kwake,  nikasema kwanini nikagawe mitungi ya gesi  uchochoroni, najua ni kidogo lakini kila mtu ajue Rais wake amemkumbuka, hivyo tumegawa kwa uwazi ili watu waione, watakaopata watashukuru na wasiopata tutatafuta mingine" amesema.


Aidha amesema ugawaji huo wa mitungi ni sehemu ya kuhamasisha kampeni  ya nishati safi ya kupikia ambayo inafanyika nchi nzima huku akifafanua katika kuendeleza jitihada hizo tayari Rais Samia amewekeza, kwani kuna mradi wa kuzalisha gesi yetu wenyewe kutoka Mtwara , na tayari mikataba ya awali imeshasainiwa.


"Pale Ikulu Chamwino Dodoma tulienda kushuhudia utiwaji saini mkataba wa kuwekeza kiwanda cha kuchakata gesi ya LNG kule Lindi ile gesi itakapokamilika itakuja mpaka Kondoa, ni ndoto yake Rais  na sisi tukimuunga mkono na kumuongeza ataitimiza. Tutakuwa na gesi majumbani kwetu."

Post a Comment

0 Comments