Kigoma yafungua soko la kimataifa mpakani Buhhigwe



Na. Mwandishi wetu, Buhigwe

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amefungua Soko la kimkakati Mnanila  lililopo Kata ya Mnanila wilayani Buhigwe mkoani hapa.

Ufunguzi wa Soko hilo lililojengwa kwa Thamani ya Shilingi Bil.2.5 fedha kutoka Serikali Kuu, umefanyika Leo  Oktoba 12, 2023 huku ukienda sambamba na  ziara ya Mkuu huyo wa mkoa iliyolenga kukagua miradi maendeleo na kusikiliza kero za wananchi wilayani humo.

Akizungumza na wakazi waliojitokeza kwenye ufunguzi wa Soko hilo lililopo mpakani mwa Tanzania na Burundi, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wanufaika wa mradi huo kuitumia vizuri fursa hiyo kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi.

Aidha, katika kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa Soko hilo,  Andengenye ameuelekeza uongozi wa soko kuzingatia uwazi na ushirikishwaji ili kuondoa malalamiko mbalimbali yanayojitokeza miongoni mwa wafanyabiashara.

Amewasisitiza wafanyabishara hao kuendelea kuchangia  makusanyo ili kuiwezesha Serikali kuendelea kulipanua pamoja na kulifanyia maboresho soko hilo ili kuiwezesha serikali kufanya maboresho ikiwemo upanuzi wa miundombinu na kutoa fursa ya ongezeko la wafanyabiashara katika eneo hilo.

Akiwasilisha Taarifa ya Maendeleo ya Soko hilo, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Viwanda na Biashara Halmashauri ya Buhigwe Onesphory John amesema ujenzi wa Soko hilo umelenga kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili ili kuongeza chachu ya ukuaji wa biashara katika eneo hilo.



Amefafanua kuwa jumla ya vibanda 144 vimekamilika na tayari wafanyabishara mia moja wamekamilisha taratibu zinazohusiana na zabuni za upangishaji na kupatiwa vibanda hivyo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa ameiasa jamii kujenga utamaduni wa kupima Afya ili kuepukana na usugu wa maradhi unaosababaisha baadhi yao  kujiingiza katika Imani za kishirikina ikiwemo Ramli chonganishi kufuatia kuugua kwa muda mrefu.

‘’Jengeni tabia ya kupima Afya mara kwa mara na ili mkibainika na matatizo ya kiafya muweze kupata matibabu badala ya kutuhumiana kuhusu Imani za kishirikina na kukimbilia kwa kina kamchape, hao ni matapeli  achaneni nao’’ amesisitiza.

Aidha Mkuu wa Mkoa ametumia ziara hiyo ya kikazi kusikiliza kero mbalimbali za wakazi wa Buhigwe na kutatua, kushauri na kuwaelekeza namna bora ya kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hizo.

Pia Mkuu huyo wa Mkoa amewasisitiza wakazi wilayani humo kutunza Mazingira kwa kupanda miti rafiki kwa vyanzo vya maji ili kuendelea kuutunza mto Malagarasi ambao ni chanzo kikuu cha ziwa Tanganyika.

Post a Comment

0 Comments