Rais Samia aanza ziara ya kikazi mkoani Tabora

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema ameshaiagiza Wakala wa Mbegu nchini (ASA) kuzalisha mbegu zenye ubora kwa bei ambayo mkulima ataimudu.

Rais Samia amesema lengo ni kujidhatiti kuzalisha mbegu za mazao yote hapa nchini ili kuachana na utaratibu wa kuagiza kutoka nje.

Aidha, Rais Samia amesema hayo leo wakati akihutubia wananchi wa Nzega katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Samora.

Awali Rais Samia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha wilaya ya Igunga ambacho kimegharimu shilingi bilioni 2.6  

Akihutubia wananchi wa Igunga katika mkutano wa hadhara, Rais Samia amesema Chuo cha VETA ni muendelezo wa jitihada za serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu ya ufundi itakayowasaidia kuajiriwa au kujiajiri.

Vile vile Rais Samia amesema serikali imeamua kujenga chuo cha mafunzo ya ufundi stadi katika kila wilaya nchini na kuwa na chuo kikubwa kimoja katika kila mkoa.

Hali kadhalika, Rais Samia pia amesema serikali imedhamiria kukuza ujuzi wa vijana kwani ndio nguvu kazi ya taifa hivyo vyuo vya VETA vinajengwa ili ziungane na miradi na mipango inayoanzishwa na serikali ili kujenga uchumi wa nchi.

Rais Samia ameanza ziara ya kikazi mkoani Tabora ambapo alifungua mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya mji wa Shelui, kupokea taarifa ya mradi wa umeme vijijini (REA) awamu ya 3 mzunguko wa 2 na kuzungumza na wananchi wa wilaya ya Iramba.

 

 

Post a Comment

0 Comments