Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.
Doto Biteko amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kuhakikisha kuwa wanatekeleza agizo la Rais, Dkt.Samia Suluhu
Hassan la kuendelea kutoa elimu ya mlipakodi kwa Watanzania na Wafanyabiashara
ili kuleta ufanisi katika ukusanyaji kodi, kuendelea kuweka uhusiano mzuri kati
ya Wafanyabiashara na TRA na kuhakikisha kuwa kila anayestahili kulipa kodi
nchini, anailipa bila misukosuko.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati alipokuwa mgeni
rasmi katika Sherehe ya utoaji Tuzo kwa Walipakodi Bora kwa mwaka 2022/2023
iliyofanyika tarehe 24 Novemba, 2023.
“Wafanyabiashara wanapaswa kulelewa ili walipe
kodi zaidi, wanapaswa kufundishwa umuhimu wa kulipa kodi, na kazi hii ni ya
kwenu Wizara ya Fedha na TRA na ninafurahi kwamba mnaifanya vizuri, sisi
tunawatakia kila la heri katika kuifanya kazi hiyo ili mchango wa walipa kodi
uendelee kuwa mkubwa ili tuweze kufikia malengo tunayojiwekea.” Alisema Dkt.
Biteko
Alieleza kuwa, Serikali ya Awamu Sita
itaendelea kufungua nchi ili kuvutia uwekezaji zaidi, kuweka mazingira rafiki
ya uwekezaji, pamoja na kupambana na kutokomeza rushwa ikiwemo kwenye sehemu
zinazohusisha Wafanyabiashara.
Dkt. Biteko aliipongeza TRA kwa kusimamia
vizuri zoezi la ukusanyaji mapato nchini akitolea mfano malengo waliyowekewa mwaka
2022/23 ambayo wameyafikia kwa asilimia 97.4 kwani walikusanya shilingi Trilioni
24.11 kati ya shilingi Trilioni 24.76 walizopangiwa na kueleza kuwa hiyo si
hatua ndogo hivyo TRA na Walipakodi wote wanastahili pongezi.
Aidha, Dkt. Biteko ametaka Wafanyabiashara watambue
kuwa, kazi ya kujenga nchi si ya Serikali pekeyake bali ni ya watanzania wote
hivyo amewataka kuendelea kulipa kodi ili zikajenge nchi kwa namna mbalimbali
ikiwemo ujenzi wa Barabara, Shule, Umeme, Maji, Hospitali zenye madawa na
nyenzo nyingine ambazo uwepo wake unahitaji fedha.
Dkt. Biteko alitoa pongezi kwa Wizara ya Fedha
pamoja na TRA kwa kuandaa shughuli hiyo muhimu ya kuwatambua Walipakodi na
kuwapa Tuzo kama kielelezo cha kuonyesha umuhimu wao kwa uchumi wa Tanzania.
Aliwapongeza pia Wafanyabiashara waliopata Tuzo
katika sherehe hiyo huku akieleza kuwa, kwa wale waliokosa Serikali bado
inatambua mchango wao na waone kuwa Tuzo hizo ni motisha kwao ya kuchangamkia
fursa ya kutambuliwa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.
Doto Biteko akiwa katika picha ya pamoja na Washindi wa Tuzo za Walipakodi
Bora kwa mwaka 2022/2023 zilizotolewa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyofanyika tarehe 25 Novemba, 2023 jijini
Dar es Salaam.
Washindi wa Kitaifa katika Tuzo hizo za Walipakodi Bora kwa mwaka 2022/2023 ni Benki ya CRDB (mshindi wa Tatu), Tanzania Breweries (Mshindi wa Pili), huku Mshindi wa kwanza akiwa ni Benki ya NMB.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo
ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo,
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Chande, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe.
Albert Chalamila, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba,
Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Zanzibar (ZRA),Yusuph Mwenda.
0 Comments