Makonda awasha moto Kagera aitaka TAMISEMI kutatua changamoto

 


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda amewataka mawaziri wanne akiwamo Waziri Momahed Mchengerwa (Tamisemi), Hamad Masauni (Mambo ya Ndani), Waziri wa, Profesa Makame Mbarawa (Uchukuzi) na Innocent Bashungwa (Ujenzi), kufika mkoani Kagera kutatua kero.

Huenda changamoto za miundombinu, vitambulisho vya Taifa na soko la kisasa zinazoikabili Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera zikapatiwa ufumbuzi baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda kuingilia kati na kuwataka mawaziri wanne kuzitatua.

Mawaziri walioagizwa na Makonda kwa simu ni pamoja na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), Momahed Mchengerwa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya Makonda kutua mkoani Kagera kwa ajili ya ziara leo Novemba 9, ambapo amewapigia simu baadhi ya mawaziri kutoa majibu kwa wananchi walioeleza kero zao katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mayunga Park Manispaa ya Bukoba.

Paul Makonda Katibubwa NEC itikadi na uenezi Taifa

Kabla ya Makonda kuhutubia viongozi wa mkoa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato walizungumzia na kufikisha changamoto hizo kwa katibu huyo mwenezi wakimuomba chama kiwasaidie.


kuna ujenzi wa soko kuu la Bukoba na kingo za mto Kanoni bado upo taratibu haya tumeshawasilisha Serikali tunaomba Rais Samia atusaidie ili kusonga mbele," amesema Byabato ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Mashariki.


Naye, Mwasa amesema pamoja na kutoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan lakini wanaomba pia kupewa fedha za kumalizia ujenzi wa stendi ya mkoa na soko la kisasa akisema wameshaandaa michoro na makadirio ya fedha.


"Tunaomba ukumbushe Rais Samia atupatie fedha hizi, pia tunakumbushia uwanja wa ndege uliopo ni mdogo na wananchi wameshapisha mradi huo lakini bado ujenzi wake," amesema Mwasa.


Baada ya maelezo hayo Makonda amepanda jukwaani baada ya kuitwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi na katika maelezo yake ya utangulizi mwenezi huyo alisema yeye sio mtu wa kupiga porojo bali kutafuta majawapo na ufumbuzi wa changamoto za wananchi.


Amesema ameelezwa kuwa Kagera hasa Manispaa ya Bukoba kuna changamoto za ujenzi wa soko usiokamilika, changamoto kingo za Mto Kanoni huku akihoji hadi leo wala stendi ya mabasi makubwa.


Baada ya maelezo ya hayo Makonda aliomba simu yake na kumpigia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa aliyempa miezi mitatu kukanyaga Kagera kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.


Hata hivyo, katika majibu yake Mchengerwa amemuahidi Makonda atafika Kagera Desemba mwaka huu.


"Hapa zege halilali wananchi, mheshimiwa waziri nipo Kagera wananchi wanakusikia nimetoa maelekezo ya chama kwako nimekupa miezi mitatu uje Kagera kutekeleza agizo la chama.


“Tunataka Kagera iwe na stendi, soko na kingo za mto Kanoni," amesema Makonda akizungumza na Mchengerwa kwa simu.


Akijibu maelekezo hayo, Mchengerwa amesema ameyapokea maelekezo ya CCM akisema pia ni utekelezaji wa ilani ya chama hicho tawala ya mwaka 2020 hadi 2025. Lakini pia alisema maelekezo hayo ni Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara mkoani Kagera.


Baada ya Mchengerwa, Makonda aliagiza apigiwe simu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kutoa ufafanuzi suala la vitambulisho vya Taifa (Nida) na hatua walizochukua kuhusu upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa.


Akijibu suala hilo, Masauni alianza kwa kusema tatizo la vitambulisho vya Taifa limemalizwa na Serikali akidokeza kuwa shida kubwa ilikuwa ni mkandarasi anayezalisha kadi alikuwa hajalipwa lakini sasa ameshalipwa.


"Zilitengwa zaidi ya Sh 42.5 bilioni na zote zimeshalipwa hivi tunavyozungumza hadi takwimu za leo kadi zilizoingia nchini milioni tano na jumla ya Watanzania milioni 16 ambao wana kadi. Ikifika Desemba mwaka huu watu wote watapatiwa kadi," amesema Masauni.


Mawaziri wengine waliopigiwa simu ni pamoja na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyeahidi wananchi Kagera kuzifanyia kazi changamoto za sekta zao za barabara na bandari.


Katika mkutano huo wa hadhara uliohitimishwa karibia saa moja usiku Makonda alisema Rais Samia ni kiongozi asiyetokana na kundi lolote bali kundi lake ni CCM asitokee waziri, mjumbe wa halamshauri kuu au nec wala mtendaji wa kata anayebagua wananchi.

Post a Comment

0 Comments