Mradi wa Bomba la mafuta Uganda hadi Tanzania kukamilika 2025

 


Na Theresia Lugwisha- Tanga

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea kituo Bandari Chongoleani cha Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) na kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.

 

Kamati hiyo imetembelea Novemba 13, 2023 na kufanya ukaguzi wa mradi huo katika kituo kikuu cha kupokea na kuhifadhi mafuta ghafi Chongoleani, jijini Tanga.

 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. David Mathayo, ameongoza kamati katika ziara hiyo huku ikionesha kufurahishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa EACOP kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, jijini Tanga.

 

"Lengo la kamati ni kutembelea  mradi huu na kujionea kasi ya ujenzi na kwa kweli tumefurahishwa sana na kasi ya ujenzi. Tulikuja mwaka jana tukajionea maendeleo, lakini leo tumekuta mambo tofauti kabisa, maendeleo ya ujenzi yamekua kwa kasi kubwa sana," amesema  Mhe. Dkt. Mathayo.

 

Amewataka wananchi kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi huo, akiutaja utasaidia kuongeza Pato la Taifa pindi utakapokamilika Desemba 2025.

 

"Mradi huu ukikamilika utasaidia kuongeza Pato la Taifa na ajira, hivyo nitoe rai hasa kwa wakazi wa maeneo ambayo mradi huu unapita wachangamkie fursa zitokanazo na mradi ili waweze kuongeza kipato cha familia zao," alisema Mhe. Dkt. Mathayo.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. David Mathayo

 

Mwenyekiti huyo pia amesisitiza kuwa mradi huo ni muhimu utekeleze miradi ya kijamii katika maeneo yanayopitiwa na mradi.

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka amesema Wizara ya Nishati imepokea ushauri wa kamati na itasimamia vyema utekelezaji wake.

 

Amesema hadi kufikia tarehe 31 Oktoba 2023, serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilikuwa imetoa jumla ya Dola za Marekani 207 milioni kama mchango wake kwenye  hisa ya kampuni ya EACOP, Watanzania 4,228 wameajiriwa na mradi, watoa huduma 146 wazawa walinufaika na kulipwa jumla ya Sh. 355 bilioni; wananchi 9,822 sawa na asilimia 99.2 wamelipwa fidia yenye jumla ya Sh. 35 bilioni. Hivyo, kazi inaendelea vizuri.

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mbuttuka, pia amesema kazi ya ujenzi wa mradi huo inaendelea kwa kasi. Utakamilika na kuanza kufanya kazi Desemba 2025 

 

 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dkt. David Mathayo (wa pili kushoto) akiongoza kamati hiyo kukagua maeneo ambayo Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) unatekelezwa katika eneo la Chongoleani, jijini Tanga tarehe 13 Novemba, 2023.

"Mradi huu mpaka sasa umefikia sehemu nzuri na ajira zilizopo zimewapa kipaumbele zaidi wakazi wa maeneo ambayo mradi huu unapita, lakini pia tunatarajia kuona fursa nyingi zaidi zikiendelea kuchangamkiwa na wananchi, mradi huu utakamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo Desemba 2025," amesema Mbuttuka.

 

Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dkt. David Mathayo. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, (aliyemwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.) Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pia walikuwa sehemu ya ziara hiyo katika mradi wa EACOP.

 

Post a Comment

0 Comments