Bilioni tano zakusanywa kusaidia wananchi wa Hanang- Dr. Samia


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekabidhiwa hundi yenye thamani ya shilingi Bilioni 2 kutoka kwa taasisi za umma kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya ardhi yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Ikulu, Chamwino ambapo Rais Samia amekabidhiwa hundi hiyo kutoka kwa Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu kwa niaba ya taasisi mbalimbali za serikali.

Aidha, Rais Samia amesema lengo la kuwachangia waathirika hao ni kuweza kuwapatia mahitaji muhimu ili waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Hali kadhalika, Rais Samia ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kukamilisha tathmini ya maafa hayo kwa waathirika ili serikali ianze mchakato wa kuwarejesha katika makazi rasmi.

Rais Samia amewataka Watanzania kutunza mazingira kwa kusafisha na kuacha kutupa takataka katika mitaro na kuhakikisha inazibuliwa kwa wakati ili mvua zinaponyesha iweze kutiririsha maji. 

Kwa upande mwingine, Rais Samia amezishukuru taasisi za umma, wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kwa kuonesha mshikamano katika kusaidia waathirika wa maafa hayo. 

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Taasisi za Umma wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama.

Imeandikwa Na. Mwandishi wetu, Dodoma

Post a Comment

0 Comments