Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi, utenguzi na uhamisho wa viongozi kama ifuatavyo:
A: Uteuzi na Utenguzi
Amemteua Balozi Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda.
Amemteua Ndugu Selwa Abdalla Hamid kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Ndugu Hamid anachukua nafasi ya ndugu Athman Francis Msabila ambaye amesimamishwa kazi.
Kabla ya uteuzi huu, ndugu Hamid alikuwa Meneja Miradi, Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Amemteua Ndugu Mariam K. H. Chaurembo kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Ndugu Chaurembo anachukua nafasi ya Ndugu Lena Martin Nkya ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Kabla ya uteuzi huu, ndugu Chaurembo alikuwa Afisa Utumishi Mkuu, Wizara ya Nishati na amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’wale.
Amemteua Ndugu Fabian Manoza Said kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Momba. Ndugu Said anachukua nafasi ya Ndugu Butamo Nuru Ndalahwa ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Kabla ya uteuzi huu, Ndugu Said alikuwa Afisa Usimamizi Mkuu wa Mitihani, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa na amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
Amemteua Dkt. Khamis Hassan Mwinyimvua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Tanzania. Dkt. Mwinyimvua ni Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Prof. Longinus K. Rutasitara ambaye amemaliza muda wake.
B: Uhamisho
Amemhamisha kituo cha kazi Dkt. Peter Maiga Nyanja, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Muleba kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe.
Ndugu Nyanja anachukua nafasi ya Ndugu Maryam Ahmed Muhaji ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Manyara.
Uteuzi na uhamisho huu unaanza tarehe 18 Desemba, 2023.
0 Comments