*Wajumbe wa Halmashauri Kuu wataka maelezo ya kina utatuzi wake, Mawaziri wajieleza, ufuatiliaji kufanyika kwa karibu zaidi
Na. Mwandishi wetu
HALMASHARI Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Chama
Cha Mapinduzi (CCM), imeelekeza kupatiwa ufumbuzi wa haraka wa kero ya kukatika
kwa umeme, upungufu wa mafuta ambao huwa unajitokeza ingawa si mara kwa mara na
changamoto ya bei ya mazao ya kilimo.
Pia, katika kikao cha NEC kilichofanyika Novemba
29, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, wajumbe walijadili kuhusiana na huduma za
afya, hususani kwa wazee, wajawaziti na watoto, pamoja na mpango
wa bima ya afya kwa wote.
Hayo yalielezwa Novemba 30, 2023 na Makamu
Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, alipozungumza na wananchi
wa Jimbo la Rufiji, mkoani Pwani, katika mkutano ulioandaliwa na mbunge wa
jimbo hilo, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, kueleza utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.
"Chini ya Mwenyekiti Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan, kile kikao (NEC) kilifanyika siku nzima, mambo yote tuliyojadili
ni yale yaliyohusu wananchi, tulijadili kuhusu kukatikatika kwa umeme, tatizo
la mara moja moja la upungufu wa mafuta, tatizo la bei ya mazao; korosho,
pamba, tumbaku, kahawa, alizeti na mengine yote," alisema Kinana.
Alisema, Rais Dkt. Samia alimtaka Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, kutoa majibu ya hoja zilizotoka kwa wajumbe wa NEC ambapo
alifanya hivyo, akisaidiwa na mawaziri wakiwemo Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigilu
Nchemba, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
Ndugu Kinana, alisema kwamba wajumbe wa kikao
hicho walizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa upande wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Alisema, Mwenyekiti wa CCM Dkt. Samia, alimtaka
Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla
kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa ilani.
Kinana alisema, Mwenyekiti alisisitiza changamoto
zilizozungumzwa na wajumbe wa NEC kuhusiana na sekta mbalimbali zipatiwe
ufumbuzi mapema iwezekanavyo kama alivyowahi kuagiza siku za nyuma.
"Mambo haya utekelezaji wake utafuatiliwa
kwa karibu na Mwenyekiti mwenyewe," alisisisitiza Makamu Mwenyekiti Kinana.
0 Comments