Mkoa wa Kigoma umetangazwa kushinda nafasi ya pili katika tuzo za umahiri za uandaaji bora wa hesabu ngazi ya mkoa zinazoandaliwa na bodi ya taifa ya wahasibu na wakaguzi nchini (NBAA) kwa kile kilichosemwa kuwa ni uongozi bora.
Akitoa ufafanuzi wa tuzo hizo CPA Johnson Gamba mhasibu mkuu wa mkoa wa Kigoma amesema ushindi wa tuzo hizo unatoa chachu kwa jamii na wadau wa maendeleo kuamini kuwa fedha zinazotolewa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo zinatumika vizuri.
"Tumeshinda tuzo hizo kwa miaka mitano mfululizo tangu tulipoanza kupeleka taarifa zetu kukaguliwa mwaka 2018, ambapo kwa miaka mitatu mfululizo 2018/2020 tulishika nafasi ya kwanza na kwa miaka miwili ya 2021/2022 tumeshika nafasi ya pili, tunajipanga kuongeza mafunzo zaidi kwa watendaji ili waendelee kufanya vizuri na kuibuka kidedea" Amesema Gamba.
Mhasibu mkuu wa mkoa wa Kigoma ACP Gamba akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake juu tuzo Bora ya uandaaji bora wa mahesabu.
Aidha Gamba ameongeza kuwa katika halmashauri za mkoa wa Kigoma halmashauri ya wilaya ya Buhigwe imeongoza pia kwa kushika nafasi ya pili kati ya wilaya zilizokagiliwa na kuzitaka halmashauri zote kuboresha mahesabu yake na kushiriki mashindano ya tuzo hizo zinazofanyika kila mwaka nchini.
Amesema kushiriki katika tuzo hizo kutasaidia kuboresha uwajibikaji na kukamilisha malengo ya serikali ya kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Sambamba na hilo mkoa wa Kigoma pia umepokea tuzo kutoka wizara ya kilimo ya ushindi wa pili kwa uzalishajii wa mazao yasiyo ya nafaka katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 jambo linaloonesha ukomavu katika kilimo bora.
Kufuatia tuzo hiyo Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thibias Andengenye amewaagiza maafisa ugani kuwa karibu na wakulima na kuongeza kasi ya utowaji wa elimu ya kilimo bora kwa wananchi ili mkoa ufanye vizuri zaidi.
Mwandishi: Adela Madyane
Mhariri: Prosper Kwigize
0 Comments