Mwenyekiti wa Soko la chakula la Nazareti lililopo mtaa wa Ujenzi manispaa ya Kigoma Ujiji Sadock John ameiomba serikali mkoani Kigoma kuhakikisha zoezi la kuzoa taka katika vizimba linafanyika mara tatu kwa wiki ili kuondoa kero ya uchafu iliyopo katika maeneo ya Soko hilo.
Amesema hayo leo katika maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika ambapo kimkoa yamefanyika kwa kupanda miti ya michikichi 2000 katika barabara ya zamani ya Kasulu yenye urefu wa km 9 katika eneo la uwekezaji wa KISEZ sambamba na kufanya usafi katika Soko la Nazareti.
Amesema uchafu huwa unakaa muda mrefu bila kuchukuliwa na wahusika jambo linalosababisha taka kurudi sokoni pindi mvua zinaponyesha na kusababisha kero kwa wananchi.
Viongozi wa serikali wameahidi kutatua changamoto hiyo na kuwahimiza wananchi na watumiaji wa soko hilo kuzingatia usafi na kutunza mazingira
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwekeza nguvu zao katika kufanya kazi na kutafuta maendeleo ili kupiga vita ujinga, umaskini na maradhi na kuweka kando maneno na siasa ambazo zitawagawa na kupoteza ndoto za maendeleo.
Amehimiza jamii kuishi katika umoja na kulinda miundombinu ambayo awamu zote sita za uongozi zimepambana kuimarisha katika sekta zote ili iwasaidie kupata maendeleo kwa urahisi na haraka.
0 Comments