Andengenye apiga mkwara Kakonko kumaliza ujenzi wa wodi Jan 2024.


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amemuaguza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kakonko kukamilisha ujenzi wa wodi tatu katika Hospitali ya wilaya hiyo ifikapo Januari 2024 ili kuruhusu upatikanaji wa huduma ya kulaza wagonjwa.

Ametoa maelekezo hayo alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa wodi tatu mpya katika Hospitali ya wilaya hiyo zinahusisha wodi ya wanaume, wanawake na watoto na kutaka mradi huo ukamilike kwa wakati ili kuondoa adha ya wananchi kwenda kupata huduma ya kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Kibondo, takribani kilomita 46 kutoka Wilayani hapo.


"Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutatoa fursa kwa wananchi kupunguza gharama za usafiri kutoka Kakonko kwenda Kibondo pamoja na gharama nyingine zinazohusiana na matibabu" Amesema Andengenye.

Aidha mkuu wa mkoa amewakumbusha watendaji kulinda miundombinu pamoja na vifaa tiba ili kuyafikia malengo ya serikali ya awamu ya sita ya kutoa huduma bora za kiafya na kuzifikisha kwa wananchi kote nchini na kuwataka wahudumu wa afya kuendelee kuwahudumia wagonjwa kwa upendo, uvumilivu, huruma na kujituma bila kusimamiwa na mtu.

Hata hivyo, Andengenye amemshukuru Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya mkoani Kigoma kwa kuongeza idadi ya hospitali hadi kufikia 11,vituo vya afya 42, pamoja na Zahanati 254.

Kwa upande wa mkurugenzi wa Wilaya ya Kakonko Ndaki Mhuli amesema ujenzi wa wodi hizo upo katika hatua ya uwekaji wa milango, uunganishaji wa mfumo wa maji taka, upakaji rangi pamoja na uwekaji wa samani za ndani na kuahidi kuwa mradi huo utakamilika ifikapo Januari 2024.

Mwandishi: Adela Madyane

Mhariri: Prosper Kwigize 

Post a Comment

0 Comments