REA na TANESCO wapewa somo mahususi kuepuka kero kwa wateja

Watakiwa kutobeba changamoto za Wakandarasi wabovu wachukulieni hatua

Na. Mwandishi wetu, Tanga

 

Naibu Waziri wa Nishati  Mhe.  Judith Kapinga amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kutobeba changamoto za wakandarasi wabovu na wanaolegalega katika kutekeleza Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini  badala yake wawachukulie hatua kwa mujibu wa mikataba uliowekwa.

 

Mhe. Kapinga amesema hayo tarehe 6 Desemba, 2023 wakati wa ziara yake mkoani Tanga ya kukagua Maendeleo ya Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini katika Wilaya ya Korogwe, ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa REA na TANESCO wakibeba changamoto hizo, inasababisha wananchi kufahamu kuwa wao ndiyo wenye matatizo.

 

Mhe. Kapinga amelazimika kusema hayo kufuatia kuwepo kwa mkandarasi wa Kampuni ya TONTAN kutounganisha umeme katika baadhi ya vijiji na vitongoji vya  Wilaya ya Korogwe Vijijini kwa sababu mbalimbali.

 

Amesema Serikali imejitahidi sana kumsimamia huyo mkandarasi, imekaa naye mara nyingi ili kuona atamaliza lini kazi, lakini mkandarasi analegalega na siyo muungwana kwa sababu amepewa kazi ya kuunganisha watanzania ambao wanamahitaji ya umeme ili kuboresha hali zao za kiuchumi na bado ameendelea kulegalega  hivyo hawatendei haki watu hao kwa sababu wanataka umeme ili waboreshe maisha yao.

 

"REA na TANESCO acheni kubeba changamoto za wa kandarasi wabovu na wanaolegalega kwa kuwa wananchi wanaona kuwa ninyi ndiyo wenye shida , msiwakingie vifua wala kuwatatulia changamoto zao hayo siyo matatizo yenu ni matatizo ya mkandarasi asiye muaminifu na hatutakubali  mkandarasi mbovu aturudishe nyuma, TANESCO na REA kazi yenu ni kuwapa kazi wakandarasi na kazi hiyo inatakiwa kuisha desemba 2023 siku chache zimebaki kuanzia sasa", amesema Mhe. Kapinga.


Mkandarasi wa Kampuni TONTAN, Mhandisi Lomayan Mollel akiwaeleza Wakazi wa     Kata ya Mbuyuni namna atakvyokamilisha Mradi wa Usambazi Umeme katika Kijiji hicho, Wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga tarehe 6 Desemba 2023, Wilayani Korogwe Vijijini Mkoani Tanga.

 

Mkandarasi huyo alitakiwa kumaliza kazi desemba  30 mwaka huu, lakini mpaka sasa takribani siku 24 zimesalia mkandarasi huyo bado hajamaliza kazi, hivyo amewataka REA kutompa kazi tena Mkandarasi huyo hata kama atamaliza kazi hiyo kwa muda uliosalia na Serikali iko kazini kuhakikisha mkandarasi huyo anatekeleza kazi yake kwa mujibu wa mkataba.

 

Amewataka Wakandrasi kuacha tabia ya kusingizia mvua, barabara mbovu ama eneo la milimani kwakuwa wakati wakipewa mkataba wa kazi hayo yote yalifahamika.

 

Naibu Waziri wa Nishati Mhe.Judith Kapinga akiwa na  Watoto wa Hamasa waliofika kumlaki katika Kata ya Makuyuni Kijiji cha Sharaka Wilaya ya Korogwe Vijijini alipofanya ziara ya kukagua Maendeleo ya Utekelezaji wa Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini, tarehe 6 Desemba, 2023.


Alisisitizakuwa Agenda ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kujali wananchi kwa kuwaleta maendeleo, ndiyo maana Viongozi wanakwenda wenyewe kuangalia utekelezaji wa miradi, kuwasikiliza wananchi ili kutatua changamoto zao.

 

"Kwa hatua tuliofikia Umeme si anasa tena ni hitaji la kila Mtu na ndiyo maana Serikali inapeleka Huduma kwa kila Kitongoji na Kijiji kuwafikia wananchi wote ili waweze kujiendeleza kiuchumi na kuleta maendeleo", Amekaririwa Mhe Kapinga.

 

Aidha amewataka wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya umeme ili isiibiwe wala kuharibiwa na watu wachache wasiopenda maendeleo kwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miundombinu hiyo.

 

Vilevile amewataka kuonyesha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuwa haina fidia ili itekelezwe kwa haraka. 

Post a Comment

0 Comments