Sherehe za Uhuru wa Tanganyika kuadhimishwa kila wilaya

 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza maadhimisho yafanyike Kitaifa kwa kuzindua mchakato na kuandikwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 - 2050 na kimkoa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo makongamano ya kujadili hatua za maendeleo yaliyofikiwa. 

 

Hayo yamesemwa leo (Jumapili, Desemba 3, 2023) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na maelfu ya wananchi na viongozi wa mikoa na wilaya waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya Bibi Titi Mohammed kwenye viwanja vya Ujamaa, Ikwiriri, wilayani Rufiji, mkoani Pwani. 

 

"Tarehe 9 Desemba, 2023 ni maadhimisho ya kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu ambapo mwaka huu Taifa letu litaadhimisha miaka 62. Mwaka huu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameagiza maadhimisho yafanyike Kitaifa kwa kuzindua mchakato na kuandikwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 - 2050 na kimkoa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo makongamano ya kujadili hatua za maendeleo yaliyofikiwa kupitia kaulimbiu isemayo “Miaka 62 ya Uhuru: Umoja na Mshikamano ni Chachu ya Maendeleo ya Taifa letu.”

 

Amesema: "Kila mkoa umeombwa uandae wazee watano maarufu ili waweze kushiriki tukio hilo litakalofanyika Ikulu lakini pia mwaka kesho Muungano wetu utatimiza miaka 60. Kwa hiyo, tunajiandaa na sherehe za miaka 60 ya Muungano ambazo kitaifa zitafanyika Zanzibar," amesema. 

 

Mapema, Waziri Mkuu alikabidhi magari 22 kwa Wakuu wa Mikoa wanne na Halmashauri mbili ikiwa ni uwakilishi wa magari 125 yaliyokwishawasili nchini kati ya magari 528 yaliyoagizwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa gharama ya sh. bilioni 57.

 

Waziri Mkuu aliwataka wakasimamie utunzaji wa magari hayo ili yaweze kudumu na yatumike kwa malengo yalikosudiwa.

 

Wakuu wa Mikoa waliopokea magari kwa niaba ya wenzao ni wa kutoka Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Halmashauri zilizopokea magari hayo ni za Rufiji na Ruangwa. 

 

Akitoa taarifa kuhusu magari hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa alisema magari 316 kati ya 528 ni ya kubebea wagonjwa na magari 212 ni ya  usimamizi wa shughuli za afya. 

 

Alisema baada ya uzinduzi wa leo, magari hayo yatasambazwa kwenye mikoa mingine.

Post a Comment

0 Comments