Tanzania yateta jambo na Uturuki katika mahusiano ya kimataifa

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amekutana kwa mazungumzo na Rais wa Taasisi ya Waturuki waishio Nje ya Uturuki na Jamii zao (YTB) Bw. Abdullah Eren katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mbarouk ameiahidi Taasisi hiyo kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Uturuki kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.

 

Amesema uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki ni wa muda mrefu na unaoongoza hasa katika sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji na kuelezea matumaini yake kuwa uhusiano huo utaendelea kuimarika zaidi.

 

Naye Bw. Eren amesema YTB ni Taasisi ya Uturuki inayojihusisha na utoaji fedha za ufadhili katika ngazi ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa mataifa mengine na kusaidia juhudi za mtangamano za Diaspora wa Uturuki  wanaoishi nje ya nchi hiyo.

 

Mazungumzo ya viongozi hao yamelenga kuimarisha uhusiano zaidi katika sekta ya elimu kati ya Tanzania na Uturuki na Mkutano huo umewezesha kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande mbili ikiwa ni pamoja na kuona jinsi ushirikishwaji wa diaspora unavyovyoweza kuchangia maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiutamaduni katika nchi husika.

 

Katika tukio jingine, Balozi Mbarouk amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Yahya Ahmed Okesh na kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya mataifa yote mawili.

Post a Comment

0 Comments