Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wakazi wa mji mdogo wa Katesh walioathirika na mafuriko makubwa kuwa serikali itarejesha huduma zote za msingi za kijamii.
Rais Samia amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufanya tathmini ya uharibifu wa mali huku akiiagiza Wizara
ya Nishati kuangalia uwezekano wa upatikanaji wa umeme wa dharura baada
ya miundombinu kuharibika na maafa haya ili shughuli za uopoaji zifanyike usiku
na mchana.
Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi na waathirika mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo na kushuhudia hali halisi ya uharibifu wa maafa.
Aidha Rais Samia ameongeza kuwa mbali na michango
mbalimbali iliyotolewa ndani ya nchi lakini pia kumetolewa takriban Shilingi
bilioni 2.5 kutoka kwa wahisani walioshiriki kwenye mkutano wa COP 28, Dubai.
Miongoni mwa maeneo aliyotembelea Rais Samia ni Hospitali ya Tumaini wilayani humo kwa ajili ya kuwajulia hali na kuwafariji majeruhi na pia shule ya Sekondari ya Katesh ambapo ndipo makazi ya muda yalipowekwa ili kuwastiri waathirika hao.
Vile vile, Rais Samia ametaka tahadhari zote za msingi zichukuliwe ili kusitokee janga jingine la mlipuko wa magonjwa hivyo kuheshimu kanuni za usafi kwani amesema majanga wakati mwengine huzua maradhi kama kipindupindu.
Hivyo Rais Samia ameielekeza
Wizara ya Maji kuhakikisha huduma za maji safi na salama zinaendelea kupatikana
muda wote huu hususan maeneo yaliowekwa makambi ya kustiri waathirika wa janga
hilo.
Mafuriko mazito yaliotokea
yamesababisha vifo vya Watanzania 76 hadi sasa, huku kaya 1,150 zikiwa
zimeathirika na watu 5,600. Pia kumekuwa na majeruhi zaidi ya 117 pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara,
maji na umeme.
0 Comments