Wizara ya mambo ya nje yafanya tukio nyeti kwa ajili ya Afrika

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Mussa Shaib amefungua Semina ya Ngazi ya Juu kuhusu Afrika tunayoitaka inayojadili fursa na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika masuala ya maendeleo.


Akifungua semina hiyo Balozi Said amesema Tanzania imejidhatiti kutekeleza Ajenda 2063 na Ajenda 2030 kwakuwa imeziweka katika mipango ya maendeleo ya kitaifa na kufanya ajenda hizo kutekelezwa kwa vitendo kupitia mipango ya maendeleo.


“Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo umasikini, ukosefu wa maendeleo, ajira, amani na usalama, kutokuwa na sauti moja katika majukwaa ya kimataifa, nchi za Afrika lazima ziendelee kupambana ili kuhakikisha Afrika inayotakiwa inafikiwa” alisema Balozi Said Mussa 
Shaib.


Amesema Tanzania imepiga hatua katika kutekeleza malengo ya Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 na hivyo kuendelea kuimarika kwa kiwango cha ukuaji ambacho alisema kuwa kinatarajiwa kuendelea kukua kwa zaidi ya asilimia 5 kwa mwaka 2024 na kuendelea. 


Amebainisha kuwa kiwango hicho cha ukuaji kimechochewa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu na uwekezaji inayotekelezwa na Serikali katika sekta mbalimbali. Ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Barabara, Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere pamoja na urekebishaji wa miundombinu ya bandari na viwanja vya ndege nchini.


Ameeleza kuwa Tanzania imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kilimo ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kutokomeza njaa nchini na kuongeza kuwa hatua kadhaa zimechukuliwa kuimarisha upatikanaji na usawa katika Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ufundi (TVET) na elimu ya juu. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Mussa Shaib

Aidha Balozi Said amefafanua kuwa Tanzania pia imefanikiwa kupunguza viwango vya vifo vya mama na watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huku ikiendelea kufurahia amani na utulivu kwa kuboresha demokrasia, utawala bora, haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria.


“Mbali na mafanikio niliyoyaeleza, bado nchi wanachama zinakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063 na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 na hivyo taarifa za tathmini katika nchi mbalimbali zinaonyesha utendaji wa jumla uko katika kiwango cha wastani” alisema Balozi Mussa.


Ametaja baadhi ya sababu zinazochangia utekelezaji wa ajenda hizo kuwa wa kiwango cha wastani kuwa ni pamoja na utawala dhaifu, mifumo mibovu ya usimamizi na uratibu kati ya wahusika wa maendeleo wa ndani na nje katika ngazi ya nchi, pamoja na rasilimali zisizotosha. 


Ameishukuru Ofisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha utekelezaji wa Malengo ya Milenia yanaendelea kufanyiwa kazi na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Ofisi hiyo  ili  kufikia  malengo hayo kwa ukamilifu.

Semina hiyo imeandaliwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Barani Afrika (UNECA) inajadili utekelezaji wa Agenda 2063 na Agenda 2030 katika ngazi ya Nchi  na Mpango wa utekelezaji wa Miaka 10 wa Ajenda 2063 ambao utatoa ramani ya mabadiliko ya Bara la Afrika ndani ya muongo mmoja kama ulivyopitishwa na Mawaziri wa Umoja wa Afrika mwezi Oktoba 2023

Post a Comment

0 Comments