Askofu wa kanisa la Anglikana jimbo la magharibi
Kasulu (Diocese of western Tanganyika) mhashamu Emanuel Bwata ametoa wito kwa
serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti vitendo vya kishirikina na uporaji
vinavyofanywa na watu wanaojiita kuwa kundi la kamchape
Wito huo ameutoa leo wakati wa ibada maalumu ya
kumbukizi za kuanzishwa kwa jimbo hilo iliyofanyika katika kanisa kuu la
mtakatifu Andrea mjini Kasulu ambapo Mkuu wa Wilaya Kanali Isack Mwakisu, Profesa
Joyce Ndalichako mbunge wa jimbo la Kasulu mjini pamoja na Josepbine Genzabuke
mbunge wa viti maalumu walikuwa sehemu ya waumini katika kanisa hilo.
Askofu Bwata amebainisha kuwa kikundi hicho
kinaendesha wizi, uporaji na unyang’anyi wa mali na kuchochea chuki miongoni
mwa wanajamii kwa kisingizio cha kutoa uchawi majumbani huku wakijinasibu kuwa
na mamlaka juu ya mtu yeyote.
“Ukimya wa serikali dhidi ya hao wanaojiita
kamchape ndio unaowapa nguvu za kuendelea kutenda uhalifu huo unaochochea chuki
na udhalilishaji kwa jamii, mbaya zaidi wanataja kuwa na vibali kutoka juu,
ikiwemo kuhusisha jina la Rais” Anaeleza Askofu Bwata.
“Tunajua wapo wachawi na wapo wagaga wa jadi ambao
hutenda mambo yao kulingana na Imani yao, kazi yetu sisi ni kuwahubiria neno la
Mungu ili wamfuate Yesu, lakini hao kamchape siyo waganga maana vitendo vyao ni
vya uporaji wa mali za wananchi” Anasisitiza Askofu Bwata.
Katika hatua nyingine Askofu Bwata ametoa wito wa
kufanyika kwa chaguzi za viongozi wa serikali kwa kizingatia maadili na kuepuka
vitendo vya rushwa miongoni mwa wagombe.
“Ni aibu na dharau kubwa kwa wananchi kumchagua mtu
ambaye anahonga chumvi na mavazi hususani fulana, kofia na vitenge badala ya
kujenga hoja na kutangaza sera juu ya namna atakavyowatumikia wapiga kura, mimi
kama askofu katika huduma zangu baada ya tume ya uchaguzi kutangaza kuanza kwa
mchakato wa uchaguzi, nitawafundisha na kuwaelekeza waumini njia sahihi za
kupata viongozi bora” Amesisitiza Askofu Bwata.
FUATILIA MJADALA KWENYE TWITTER YA BUHA FM RADIO HAPA
Aidha askofu Bwata ametumia muda huu kuitaka serikali
kuwaacha huru wananchi kugombea na kuchagua viongozi wanaowataka bila kujali
wanatoka vyama gani vya siasa akitaja kuwa hiyo ndiyo demokrasia sahihi.
Amehitimisha hotuba yake kwa kutoa wito kwa serikali
kuweka wazi mchakato wa maoni ya sheria za uchaguzi, mchato wa Katiba mpya na
sheria za vyama wa siasa akidai kuwa sheria pamoja na katika ni mali ya
wananchi hivyo uwepo uhuru kwa kila mwananchi kushiriki badala ya wanasiasa
kugeuza michakato na mipango ya serikali kama mali yao.
Akijibu baadhi ya hoja za Askofu Bwata, Mkuu wa wilaya
ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu amewaeleza wananchi wa Kasulu kuwa serikali
hairuhusu vitendo vya Kamchape na hatua mbalimbali za kisheria zimekuwa
zikichukuliwa dhidi ya wafuasi na mashabiki wa kikundi hicho
“Serikali haiungi mkono uhalifu na hao kamchape ni
wahalifu, Rais Samia hajawatuma na hawezi kufanya upuuzi huo, hao ni wahalifu
na wanatoa kauli hizo ili kuichafua heshima ya Rais na heshima na amani ya nchi
yetu, hivyo wapuuzeni” amesisitiza Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack
Mwakisu.
Kanali Mwakisu ametoa onyo kwa wanaojihusisha au
kushabikia Kamchape kuacha mara moja, huku akitoa wito kwa wananchi kutoa
taarifa kwa mamlaka za serikali ikiwemo vyombo vya dola endapo watawabaini
wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Naye Mbunge wa jimbo la Kasulu mjini Profesa Joyce
Ndalichako aliyekuwa mgeni rasmi katika Ibada hiyo amelipongeza kanisa la
Anglikana kwa namna wanavyotoa ushirikianoo kwa serikali katika kutekeleza afua
mbalimbali za maendeleo Pamoja na kuhubiri amani
Profesa Ndalichako amebainisha kuwa kanisa lina
mchango mkubwa katika kuisaidia serikali kutekeleza wajibu wake wa kuhudumia
wananchi na kuimarisha usalama katika jamii nan chi kwa ujumla.
Akieleza kuhusu masala ya ajira, Ndalichako amewajulisha
watanzania kuwa serikali inaendelea na mipango yake ya uwezeshaji jamii
kiuchumi kupitia Nyanja mbalimbali ikiwemo mfuko wa asilimia 10 za mapato ya
ndani ya halmashauri ambao hutoa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu ambao wameanzia vikundo na miradi ya maendeleo.
“Serikali inaendelea na maboresho mbalimbali ya mifuko
ya uwezeshaji jamii kiuchumi, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kubuni mradi na
kufanya kazi kwa bidi ili kujiletea maendeleo na kuepuka utegemezi” amebainisha
Prof. Ndalichako Mbunge
Amesisitiza kuwa miradi ya kimkakati inayoendelea
kujengwa wilayani Kasulu na katika mji wa Kasulu ukiwemo umeme, Barabara na
maji, ni sehemu tu ya mipango ya serikali kuhakikisha jamii inapata huduma za
kijamii kwa ubora zaidi.
“Nikitazama nilivyolipokea jimboa la kasulu na hali
ilivyo sasa naona fahali sana maana mambo yamebadilika na kuna miradi mingi
imefanyika hususani sekta ya afya, elimu, miundombinu na maji, sina budi kumpongeza
mheshimiwa Rais kwa utoaji wa fedha nyingi za maendeleo kwa ajili ya jimbo letu
na mkoa wetu kwa ujumla. Anabainisha Mh. Ndalichako
Kuhusu Imani za kishirikina, profesa Ndalichako ametoa
wito kwa viongozi wa kanisa kuendelea kukemea na kutoa elimu ili watu
wanaoamini ushirikiana wageuze mienendo yao.
Aidha Profesa Ndalichako amewataka wazazi kuhakikisha Watoto
wote wanaotakiwa kujiunga na shule za awali, msingi na sekondari kidato cha
kwanza kuhakikisha wanawapeleka kuanza masomo.
Kanisa la Anglikana jimbo la magharibi lenye makao
makuu mjini Kasulu, linaongoza waumini wa kanisa hiyo katika mikoa ya Rukwa,
Katavi, Tabora na Kigoma na linatimiza nusu karne tangu manisa kuu kujengwa.
0 Comments