Je! Ziara ya Rais Samia nchini Indonesia italeta mageuzi ya Mafuta na Gesi?


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Indonesia wiki hii wameshuhudia makabidhiano ya Hati za Makubaliano 4 na barua ya kusudio 1 kati ya nchi hizo mbili zinazolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi.

Rais Samia akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya Kitaifa nchini humo amesema makubaliano hayo yataimarisha miaka 60 ya kidiplomasia na uchumi kati ya tanzania na Indonesia.

Miongoni mwa masuala waliojadili viongozi hao ni namna ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji ambapo Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mkutano wa kwanza wa tume ya Makubaliano ya ushirikiano.

Pia viongozi hao walifanya majadiliano ya namna ya kuendeleza ushirikiano katika uwekezaji kwenye sekta ya mafuta na gesi huku kampuni ya Indonesia ya Pertamina ambayo ni miongoni mwa wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania ikiongeza hisa Mnazi Bay, Mtwara.

Mbali na kujenga uwezo kwa wafanyakazi wa TPDC, pia Indonesia ina nia ya kampuni yake ya ESSA kuwekeza kwenye kilimo hususan mbolea na Medco Energy kwenye upande wa nishati.

Kwa upande wa sekta ya dawa, kipaumbele hasa ni Indonesia kuiuzia Tanzania dawa ambapo kipaumbele kitakuwa katika uuzaji na usambazaji wa dawa za kutibu saratani.

Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake rais wa Indonesia Joko Widodo wakihutubia baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano kadhaa ya kimkakati.

Makubaliano mengine 3 ambayo Rais Samia ameshuhudia ni pamoja na Uchumi wa Buluu, ushirikiano wa sekta ya kilimo, madini, diplomasia biashara na elimu ya juu.

Chini ya makubaliano hayo, Watanzania wanatarajiwa kuzitumia fursa zilizopo kushirikiana na wawekezaji kutoka Indonesia katika utekelezaji wa miradi lukuki inayotarajiwa kuanza na inayoendelea

Aidha makubaliano hayo yanatoa fursa kwa vijana wa kitanzania kwenda kusoma nchini Indonesia na wakati huo huo raia wa Indonesia kuja kupata elimu nchini tanzania hususani katika fani ya lugha ya kiswahili ambacho kinakuwa katika soko la elimu na uchumi wa dunia.

Hoja ni je! watanzania wamejipanga kuzitumia ipasavyo fursa hizo? Je! TPDC itafanya mageuzi zaidi katika kuhakikisha huduma za mafuta na gesi zinakuwa nafuu kwa watanzania ikiwemo kuhakikisha gesi inasambazwa nchii nzima na kupungua kwa bei? Hii ndiyo hoja ya waliowengi ili kupima tija ya ziara za Mheshimiwa rais Dr. Samia Suluhu Hassan nje ya nchi ambapo anashawishi ukuaji wa diplomasia ya uchumi.

 

Post a Comment

0 Comments