Kapinga aitaka Kampuni ya joto ardhi kuonesha matokeo chanya

Kampuni ya Uendelezaji wa Joto Ardhi Tanzania (TGDC) imetakiwa kuonesha Matokeo Chanya kwa kuzalisha Umeme kwa kutumia Rasilimali ya Jotoardhi ili kuunga Mkono Mpango wa Serikali wa kuwa na Nishati Safi na Endelevu.

 

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wakati wa kikao na Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni hiyo pamoja na Menejimenti ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukutana na baadhi ya Taasisi na Kampuni zilizo chini ya Wizara ya Nishati kwa lengo la kuona Utendaji kazi wa Taasisi hizo Tarehe 8 Januari 2024, Jijini Dar Es Salaam.

 

Mhe. Kapinga ameieleza TGDC kuwa wabunifu na kutumia uwezo wao wote kuhakikisha kuwa Kampuni hiyo inaanza kuzalisha umeme kwa kutumia Rasilimali ya Jotordhi kwa kuwa tayari baadhi ya maandalizi yameshafanyika katika maeneo ya vipaumbele.

 

Amesema kama ambavyo Serikali imejipambanua kuwa inatekeleza Mpango wa Nishati Safi na Endelevu, ni wakati wa TGDC sasa kuonesha uwezo wao katika kufanikisha hilo ili kutoa mchango mkubwa kwa Taifa.

 

Vilevile amewasisitiza kuwa ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya na ya haraka zaidi ni vyema wakaongeza ubunifuuthubutu, kushirikiana na kutoridhika nkila  wanachofanya ili kupiga hatua mbele zaidi. Hali hiyo itaondoa changamoto ya umeme unayoikumba nchi kwa kuzingatia kuwa nishati ya Jotoardhi ni endelevu.

 

Nchi na Watanzania wanataka kuona umeme unaozalishwa kutokana na Jotoardhi,TGDC ni wakati wenu sasa kuonyesha uwezo wenu wa kuleta matokeo Chanya kwa Taifa, tumieni Ubunifu na Uwezo wenu wote kuhakikisha kile mlichokikusudia kinafanikiwa na kuonekana kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inavyoelekeza kuwa uzalishaji wa umeme utaongezeka kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo Jotoardhi, vilevile kuunga mkono Mpango wa serikali wa kuwa Nishati Safi na Endelevu”, alisema Mhe. Kapinga.


Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC)wakati wa ziara ya kikazi iliyofanyika Tarehe 08 Januari, 2024 Jijini Dar es salaam


Aidha amewapongeza TGDC kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kuhakikisha umeme unapatikana na pia amewataka kutumia vyema Weledi na Taaluma walio nayo kulinda Kampuni hiyo ili kupata matokeo ya haraka.

 

“TGDC lazima muonyeshe mchango wenu Nishati Safi na Endelevu ili Nchi  na Dunia ione uwepo wenu na Serikali inataka matokeo hivyo mjikite katika hilo na watanzania wanaamini katika matokeo” alisisitiza Mhe. Kapinga.

 

Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Athumani Mbuttuka, amewaeleza TGDC kuwa ofisi yake iko wazi wakati wote ili kupokea changamoto zozote zinazowakabili ili kuwasaidia na kuzitatua pale watakapoona wanakwama katika kutekeleza majukumu yako.

 

Sambamba na hilo amewataka kushirikiana, kuwa wabunifu na wenye uthubutu kuhakikisha kile walichokikusudia kinafanikiwa na watanzania wanapata umeme.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TGDC Prof. Shubi Kaijage na Meneja Mkuu wa TGDC, Mha. Mathew Mwangomba wamemuakikishia Naibu Waziri Kapinga kuwa watashirikiana kwa pamoja kuhakikisha wanazalisha umeme wa Jotoardhi haraka iwezekanavyo na wanaendelea kutoa elimu ya Rasilimli ya Jotoardhi kwa wadau mbalimbali ili wawe na uelewa mpana zaidi kuhusu mradi huo wa kimkakati.

Wamesema kuwa kampuni hiyo ina miradi mitano ya kipaumbele ambayo ni ule wa Ziwa Ngozi unaotajiwa kuzalisha Megawati 70 lakini kwa kuanzia wataanza na Megawati 30. Mradi Mingine ni wa Kiejo- Mbaka mkoani Mbeya Megawati 60, Songwe mkoani Songwe Megawati 5 hadi 38, Luhoi mkoani Pwani Megawati 5 na  Natroni mkoani Arusha Megawati 60.

 

Miradi yote hiyo iko katika hatua mbalimbali ambapo nguvu kubwa imeelekezwa katika Mradi wa Ngozi ambapo tayari mtambo wa kuchoronga visima vya Jotoardhi umepelekwa huko na hivi karibuni wataanza kazi ya uchorongaji.

  

Post a Comment

0 Comments