Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona viongozi wote wanatatua kero na changamoto za wananchi na kwamba anasikitishwa na baadhi ya viongozi ambao hawatatui changamoto za wananchi mpaka pale anapofanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Biteko
amesema hayo tarehe 25 Januari, 2024 wakati
akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Magodi na Kigandini wilayani
Mkinga mkoani Tanga mara baada ya kuwasha
umeme katika vijiji hivyo ambao umesambazwa na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA).
Katika ziara yake kwenye Vijiji hivyo,
aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, Mbunge wa Mkinga ambaye
ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.
“Mhe. Rais
anafanya kazi kubwa katika kila Sekta na mabilioni ya pesa yamekuwa yakipelekwa
kila Mkoa kwa ajili ya kuboresha huduma za wananchi, nikitolea mfano hapa Tanga
Serikali ya Awamu ya Sita imeshaleta shilingi Trilioni 2 na Bilioni 600 kwa
ajili ya miradi ya maendeleo, kwenye umeme miradi inaongezeka kwani mmepata
bilioni 133.6 huku Wilaya ya Mkinga ikipata bilioni Nane kwa ajili ya
usambazaji umeme, Dkt. Samia anapambana ili kuwaletea maisha bora watanzania
hivyo viongozi wengine tusiishie kusikiliza kero tu bali tuzitatue na kama kuna
mahali tunahitaji watupe muda, tuwaambie kwa uwazi.” Amesema Dkt.Biteko
Katika hatua
nyigine, Dkt. Biteko amewataka Wazazi na Walezi nchini kupeleka Shule watoto
wote wanaostahili kuwa mashuleni katika kipindi hiki ambacho Shule
zimefunguliwa ili wapate elimu itakayowasaidia katika maisha yao na nchi kwa
ujumla, akitolea mfano kwa Mkoa wa Tanga watoto walioripoti Shule ni asilimia
60.
Hivyo, ameagiza
viongozi kusimamia suala hilo ikiwemo kuendesha msako na kutumia sheria
zilizopo kwa wale wanaoficha watoto ili wasiende shule kwani ifikapo mwezi
Machi watoto wote wanatakiwa wawe wameripoti mashuleni.
Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akikata utepe kuashiria
uwashaji umeme katika Kijiji cha Magodi
wilayani Mkinga mkoani Tanga tarehe 25
Januari 2024. Kulia kwake ni Mbunge wa Mkinga ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Dusntan Kitandula na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri
Kindamba.
Kuhusu usambazaji umeme vijijini, amepongeza REA kwa kuendelea kusambaza umeme vijijini akitolea mfano kuwa, usambazaji umeme vijijini mkoani Tanga umefanyika kwa asilimia 91 na wilaya ya Mkinga yenye Vijiji 85 tayari vijiji 82 vimesambaziwa umeme huku kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji vilivyosalia ikiendelea na baadaye vitafuata vitongoji.
Kuhusu hali
ya umeme nchini, amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya kila jitihada kuboresha
hali hiyo kwa kuhakikisha kuwa mitambo ya umeme inafanyiwa maboresho na miradi
mipya inaanzishwa na kutekelezwa akitolea mfano kituo cha umeme cha New Pangani
(MW 68) kinatarajiwa kuzalisha umeme
baada ya siku mbili baada ya kufanyiwa maboresho.
Akiwa katika
Kijiji cha Magodi, Dkt. Biteko amechangia shilingi milioni 5 kwa ajili ya
kusaidia kubadilisha paa la zahanati ya kijiji hicho ambalo limechakaa na
kuahidi kumalizia ujenzi wa jingo la Madrasa katika Kijiji hicho.
Kwa upande
wake, Mbunge wa Mkinga ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Dunstan Kitandula ameishukuru Serikali kwa kutekeleza kwa ubora miradi ya umeme vijijini wilayani
humo na kuwafanya wananchi kufanya shughuli za kiuchumi pamoja kuboresha utoaji
wa huduma kwenye maeneo mbalimbali kama vile vituo vya Afya na Shule.
Aidha,
ameiomba Serikali kuendelea kusambaza umeme kwenye maeneo mengine yaliyosalia
kama vile vitongojini ili wananchi
katika maeneo hayo pia wapate huduma ya
umeme.
Mwandishi: Teresia Mhagama
Mhariri: Prosper Kwigize
0 Comments