Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na
Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri kudhibiti na kutokomeza vitendo vya uvuvi
haramu.
Rais
Samia ameyasema hayo leo wakati akihutubia wananchi katika uwanja wa Nyamagana
mara baada ya kuzindua na kukabidhi boti za uvuvi na vizimba vya kufugia samaki
kwa wavuvi wa kanda ya ziwa.
Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara hiyo kuwachukulia hatua kali za kisheria wavuvi wanaokiuka taratibu za uvuvi salama.
Rais Samia pia amesema serikali inafanya jitihada
kuinua sekta ya uvuvi nchini kwa kuimarisha utendaji wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili iendane na dhamira ya mageuzi yaliyokusudiwa.
Vile vile, Rais Samia amesema kundi
la vijana na wanawake linaongoza kushiriki kwenye ajira zisizo rasmi hivyo serikali inarasimisha
shughuli zao kwa kuwawezesha kupata zana na nyenzo za kisasa ili kujikimu
kiuchumi.
Rais Samia amesema serikali imejipanga kukuza sekta ya uvuvi kupitia miradi
mbalimbali ikiwemo ununuzi wa meli za
kisasa za uvuvi katika bahari kuu, ujenzi wa bandari za uvuvi katika maeneo ya
Kilwa Masoko mkoani Lindi na Bagamoyo ili kuongeza pato la taifa.
Boti 160 za uvuvi wa kisasa zimezinduliwa kwa
wanufaika 989 pamoja na vizimba 222 vinavyotarajiwa kugaiwa kwa wanufaika 1,213
katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Geita.
0 Comments