Prof. Kitila Mkumbo atoa ahadi nzito kwa makampuni ya Simu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni za simu nchini kwa kuwa kampuni hizo zimekuwa wadau wakubwa wa maendeleo. 

Ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mkuu wa Masoko ya Kimataifa wa Vodacom, Bw. Diego Gutierrez.

“Mhe. Rais ametengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji na hivyo ni wajibu wenu wawekezaji kuwa waadilifu, kulipa kodi inavyotakiwa kwa kuwa pia tunataka kampuni zikue. Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana nanyi kwa kuwa mnatoa ajira kwa watu wetu na nyie Vodacom mnaendelea kulipa kodi vizuri”, ameeleza Prof. Mkumbo. 

Aidha, Prof. Mkumbo amebainisha kuwa wakati huu ambao Serikali inaendelea na zoezi la uandaaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, kampuni za simu ni mdau muhimu katika uelemishaji wa wananchi juu ya ushiriki wao hasa wakati wa ukusanyaji maoni. 

Waziri Mkumbo akizungumza na wadau wa mawasiliano katika kikaoo maalumu ambapo wameteta kuhusu umhimu wa kushirikiana na mitandao ya simu

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Masoko ya Kimataifa wa Vodacom, Bw. Diego Gutierrez ameishukuru Serikali kwa kushirikiana vizuri na sekta binafsi pamoja na kuendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hali inayosaidia kampuni hiyo ya Vodacom kuendelea vizuri na shughuli zake za uendeshaji nchini Tanzania na  kuwekeza zaidi.

“Ni dhahiri kuwa mafanikio haya yasingepatikana bila kuwepo kwa ushirikiano mzuri na Serikali, matarajio yetu kuendelea kushirikiana vizuri na Serikali na tunaanzisha miradi ya miundombinu kwa kushirikiana na wadau wengine hivyo tutaomba ushirikiano wa Serikali wakati wa utekelezaji wake”, ameeleza Bw. Gutierrez. 

Katika kikao hicho Bw. Gutierrez aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire na Mkurugenzi wa Masuala ya Nje na Vodacom Foundation, Bi. Zuweina Farah.

Post a Comment

0 Comments