TANAPA, REA na STAMICO waipongeza RUJAT kwa kuwatambua

Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT) kimetoa cheti cha shukrani kwa mamlaka ya uhifadhi nchini Tanzania (TANAPA), Shirika la madini la serikali (STAMICO) na wakala wa Umeme vijijiii (REA) kwa kutambua mchango wao uliowezesha kufanikisha kongamano la kimataifa la haki ya kupata taarifa 2023.


Akikabidhi cheti hicho kwa Kamishna wa Uhifadhi, Katibu wa RUJAT Prosper Kwigize ameeleza kuwa TANAPA ni mdau muhimu wa habari vijijini na RUJAT ilinufaika kwa kupata mchango uliosaidia kufanikisha kongamano lililoenda sambamba na mkutano mkuu wa wanachama.

Akipokea cheti hicho kwa niaba ya Kamshina mkuu wa uhifadhi nchini, Meneja wa TANAPA ofisi ndogo za Dodoma Kamishna Dr. Noelia Myonga ameshukuru RUJAT kwa kutambua mchango wa TANAPA katika sekta ya mawasiliano ya umma.

Dr. Myonga amesisitiza kuwa mamlaka ya uhifadhi iko tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa chama cha waandishi wa habari vijijini ili kutangaza shughuli za uhifadhi na manufaa yake kwa wananchi.

"Tunawapongeza na pia tunawashukuru Chama cha waandishi wa habari vijijini kwa kuutambua mchango wa TANAPA katika majukumu yenu ya kuhabarisha, Mamlaka ya uhifadhi itaendelea kuwaunga mkono ili habari za uhifadhi ziandikwe kwa kina na jamii ifahamu shughuli zetu na wajibu wao katika uhifadhi" Amesisitiza Dr. Myonga

RUJAT kwa upande wake imejipanga kushirikiana na wadau wa maendeleo, mashirika ya umma, serikali na jamii kuhakikisha habari za maendeleo vijijini zinaandikwa na kutangazwa

Katibu wa Chama hicho Bw. Kwigize amebainisha kuwa hadi sasa RUJAT ina wanachama zaidi ya 100 wanaofanya kazi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na kwamba idadi hiyo inatoa fursa ya habari za vijijini kuandika na kusikika kitaifa, kikanda na kimataifa.

"Tunakusudia kuhakikisha nguvu kazi ya waandishi wa habari inatumika ipasavyo kutafuta, kuchakata na kusambaza taarifa zenye maslahi kwa umma hususani zinazotangaza fursa za vivutio na faida zake kwa jamii vijijini ambao ndio wahifadhi namba moja" amesisitiza Bw. Kwigize katibu wa RUJAT

Mashirika hayo ya umma pamoja na mamlaka ya maji Mjini Tabora (TUWASA) yaliunga mkono kwa hali na mali katika kufanikisha kongamano la RUJAT mwaka 2023 lililokuwa na malengo ya kuhamasisha uandishi wa habari zenye tija na zinazogusa maslahi ya jamii vijijini.

Post a Comment

0 Comments