Timu ya kuandaa mkakati wa taifa yahitaji usaidizi



Mwenyekiti wa Timu Kuu ya Wataalamu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Prof. Lucian Msambichaka amewaomba Watanzania na taasisi mbalimbali nchini kutoa ushirikiano kwa timu hiyo katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Prof. Msambichaka amesema hayo Januari 13, 2024, Zanzibar wakati wa warsha elekezi kwa timu hiyo pamoja na kuwakabidhi nyenzo za utendaji kazi.

“Tunaomba tupate ushirikiano kutoka sehemu mbalimbali, kuanzia watu wa chini, juu, katikati, mashirika na watu wa uwezo mbalimbali watupe ushirikiano. Hii kazi inahitaji mawazo kutoka kwa watu mbalimbali, ni lazima tusikie watu wa makundi mbalimbali wanasema nini,” amesema Prof. Msambichaka.

Prof. Msambichaka amewaomba Watanzania kutoa ushirikiano mkubwa ili waweze kumaliza kazi hiyo kwa muda uliopangwa. Aidha, ameahidi kuwa, timu hiyo itafanya kile kiwezekanavyo ili kutoa kitu ambacho kinatekelezeka. Amesema, “tutafanya kile kiwezekanavyo, iwe mchana, usiku, jua kali au mvua inanyesha, ili tutoe kitu ambacho kinaweza kutekelezeka na kufikiwa”. 

Akiwakabidhi nyenzo za utendaji kazi wa uandaaji wa Dira 2050 timu hiyo ya wataalam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameitaka timu hiyo kuwasikiliza Watanzania wa makundi mbalimbali na kuwauliza wanataka Tanzania ya namna gani.

“Wasikilizeni Watanzania wa makundi mbalimbali, sikilizeni malalamiko na kero zao. Waulizeni mnataka Tanzania iweje. Katika zoezi hili la maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni lazima Watanzania wafike mahali waseme hii ni Dira yetu, na ndio maana imeitwa Dira ya Taifa na sio Dira ya Serikali,” amesema Mhe. Prof. Kitila.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni maono ya nchi kwa miaka 25 ijayo. Kila Mtanzania anatakiwa kushiriki kutoa maoni, ambapo zoezi la kukusanya maoni limeshaanza. Ili kushiriki kutoa maoni  ya Dira 2050, piga *152*00# au tembelea  http://www.dira2050portal.planning.go.tz

Post a Comment

0 Comments