huku barabara inayotoka mjini Kigoma kwenda kiwanja cha ndege cha Kigoma kufurika maji na kusababisha magari kushindwa kupita katika eneo la manguruweni mjni Kigoma
Wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo ambalo ni maarufu kwa kuuza nyama ya Nguruwe, (kitimoto) na vilabu vya pombe wameieleza Buha Media kuwa wamepata madhara makubwa kwa nyumba na vibanda vya biashara zao kujaa maji na kusababisha uharibifu wa samani hali inayosababisha kuzorota kwa uchumi katika meneo hayo.
Wakizungumza na mwandishi wa Buha News mapema leo wafanyabiashara hao walisema mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kali mnamo mwezi Disemba 2023, kipindi ambacho maji yalianza kujaa alitembelea eneo hilo na kuwaagiza kuhamisha biashara zao upande wa pili wa barabara na kuzingatia kanuni za afya ili kuepusha mlipuko wa magonjwa
Hata hivyo wanadai kuwa agizo hilo halikuenda sambamba na msaada wa kiutu kwakuwa kujaa kwa maji hayo kumeenda sambamba na mamia ya wananchi kukosa makazi na imekuwa mwiba kwao kwani baadhi yao wamelazimika kufunga biashara zao kutokana na kukosekana kwa wateja.
Mmoja wa wafanyabiashara wa kitimoto Bw. Alisoni Kinoni alisema kabla ya kupata adha ya kuingiliwa na maji katika kibanda chake alikuwa na uwezo wa kuuza nguruwe tatu kwa siku, lakini adha ilipotokea alipata hasara kwa kuharibikiwa na majokofu matatu ya kutunzia nyama na kwa sasa hana uwezo wa kumaliza nguruwe ya kg 20 kutokana na ukosefu wa wateja.
"Sioni tena thamani ya biashara ninayoifanya, tumeiomba serikali ituhamishe katika maeneo mengine lakini imekuwa changamoto kutokana na aina ya biashara tunayofanya ambayo wengine hawaikubali,tunaathirika sana, tunaomba mamlaka husika zitusaidie kuondoa haya maji ili tuendelee kufanya biashara zetu kwa amani ama la, serikali itutafutie pa kwenda" alisema Kinoni
Naye Marry Wilson alisema changamoto inayowakabili inawafanya washindwe kurejesha pesa za mikopo walizochukua benki kwaajili ya kuendesha biashara, anashindwa namna ya kuhudumia watoto wake ipasavyo na anaiomba serikali iwasaidie eneo jingine la kufanyia biashara yao kwani anaamini kuwa maji yaliyopo ni mengi na hayawezi kukauka ndani ya muda mfupi.
Bw. Kechegwa Kamanda ambaye pia muathirika wa nyumba kuzama anasema changamoto kubwa ya maji kujaa katika eneo hilo imesbabishwa na miundombinu hafifu ya barabara na madaraja na mifereji ya maji mingi kutoka Mwanga,Mlole, Mwanga Kaskazini na Mwanga Kusini kwa kuwa ni eneo la chini na maji yanaelekea katika eneo hilo na anaziomba mamlaka husika zifike katika eneo hilo ili kurekebisha mifereji itakayoruhusu maji kutoka na kusambaa.
"Nimejenga hapa mwaka 2010 kwa kutumia pesa za pensheni yangu baada ya kustaafu, sijawahi kuona maji mengi kiasi hiki, ni kweli mvua ni nyingi lakini miondombinu siyo rafiki, na barabara ipo chini, na mitaro waliyoiweka yote wameelekezea kwenye eneo la bwawani, tunaomba wahandisi wafike waangalie namna ya kutawanya maji kama hayawezi kuingia ziwani basi wayatawanye, wasiwe wahandisi wa kujenga miradi kwa siku moja" alisema Kamanda.
Kwa upande wa biashara alisema licha ya kupata changamoto hizo kwa miezi miwili sasa bado mamlaka ya mapato (TRA) wanapita kukusanya kodi badala ya kuwafikia waathirika hao na kuangalia namna walivyoathirika na kuweka sawa namna ya kulipa kodi au kusitishiwa kwa kipindi hicho.
Dereva bajaji Aidan Baraka alisema adha ya maji hayo imewafanya kubadili njia na kupita njia ambazo ni ndefu na hivyo kuamua kupandisha nauli kutoka 500-1000 kwa wasafiri kutoka Mwanga kwenda Mwasenga na Airport na kubaki shilingi 1000 kutoka Kigoma mjini kuelekea katika maeneo hayo
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Katubuka Moshi Mayengo alisema maji haya ni zao la athari za mabadiliko ya tabia nchi, kwani maji kama hayo yaliwahi kutokea miaka ya 1989-1990 ambapo barabara hiyo ilijaa maji, nyumba kuzama na ikawabidi wakazi wa eneo hilo kutumia usafiri wa mitumbwi ili kuvuka ng'ambo ya pili.
Alisema serikali ya mkoa ipo kimya na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa za kuondoa maji katika eneo hilo na kwamba pamoja na jitihada alizofanya kuwasiliana na wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) bado hakuna chochote kinachoendelea licha ya wananchi kupata madhara na changamoto ya kuongezeka kwa mbu pamoja na maji hayo kutoa harufu kali.
Akizungumza kuhusu adha ya mvua hizo kwa miundombinu na usafiri kwenda uwanja wa ndege meneja wa TARURA wilaya ya Elias Mutapima, alisema wamefanya mawasiliano na mamlaka nyingine za juu kama manispaa na serikali kuu ili wafanye kutatua tatizo marekebisho ya katika bwawa la Katubuka kwa kutoa tope, udongi, mchanga pamoja na uchafu mwingine ili kuruhusu maji mengine kuingia.
"Nashauri watu wasitupe taka ovyo kwenye mitaro ambayo mvua ikinyesha inapelea uchafu bwawani na kulifanya bonde kupunguza kina na kusababisha kujaa"alisema Mutapima
Alisema hatua nyingine walizochukua ni kuisanifu upya barabara hiyo ili waiombe serikali kutenga bajeti kwaajili ya kuongeza tuta la barabara ili maji yakiongezeka yaisiweze kukata baarabara nankuwaomba watumiaji wa vyombo vya moto waache kupima maji kwa macho na hivyo waache kutumia barabara hiyo.
Namna mkoa unavyokabiliana na mlipuko wa magonjwa hususani kipindupindu Mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba alisema timu ya wataalamu wa afya wamefika katika maeneo hayo na kutoa maelekezo kwa wafanyabiashara hao huku wahudumu wa afya ngazi ya jamii wakiendelea kupita katika maeneo hayo kuhakikisha kuwa kile walichoelekezwa kinafanyiwa kazi.
Maeneo yaliodhiliwa na maji zikiwemo nyumba za makazi ya watu sasa zimegeuka kuwa sehemu ya kuvulia samaki aina ya ngege na kambale ambapo shughuli hiyo ya uvuvi inafanya na vijana wa maeneo hayo.
Kuvurugika kwa barabara rasmi inayoelekea kiwanja cha ndege mjini Kigoma kunachafua taswira ya mkoa huo ambao ni kiunganishi cha kiuchumi na kidiplomasia baina ya Tanzania na nchi za jirani hususani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi ambao huu tumia uwanja huo kwa safari za nadani na nje ya Tanzania.
Meneja wa Wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) wilaya ya Kigoma Mhandisi Elias Mutapima amekiri kuwepo kwa athari hasi za mvua kwa miundombinu ya barabara na kueleza kuwa barabara ya Katubuka kwenda kiwanja cha ndege imekuwa ikikumbwa na maji mengi yanayoivuka na kusababisha adha kwa wasafiri na kueleza kuwa tayari timu ya wahandisi kutoka TARURA imeanza taathimini ya uharibifu sambamba na kufanya usanifu upya ili kulijenga eneo hilo upya na kuepusha uwezekano wa maji kujaa barabarani.
"Tunatambua kuwepo kwa athari za ongezeko la mvua nyingi ambazo ndiyo chanzo cha ongezeko la maji katika eneo hilo ambalo liko chini likizungukwa na miinuko inayotiririsha maji hadi bonde la Katibuka, hivyo kujaa kwa maji hayo hakusababishwi na miundombinu ya barabara bali changamoto za kijiografia na mabadiliko ya tabia nchi" Amesisitiza Mhandisi Mutapima.
Pamoja na barabara ya Katibuka-Airport kujaa maji barabara nyingine ikiwemo ya Ujiji-Katonga hadi Bangwe nayo imekumbwa na uharibifu unaotokana na ongezeko la mvua zinazosadikika kuwa za Elnino ambazo zinaendelea kunyesha pote nchini.
Mwandishi: Adela Madyane, Prosper Kwigize
-Mwisho-
0 Comments