·
Dkt. Biteko apongeza
utayari wa Benki hiyo
·
Maeneo mapya yaainishwa
·
Nishati safi ya kupikia
yapigiwa chapuo
Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo
na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki kuhusu miradi mbalimbali ya umeme
inayofadhiliwa na benki hiyo pamoja na miradi mingine ya nishati iliyo katika
mpango wa kufadhiliwa.
Mazungumzo
hayo ambayo yamefanyika tarehe 05 Februari, 2024 Jijini Dodoma pia yamehudhuriwa
na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakiongozwa na Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba.
“Benki
ya Maendeleo Afrika imeonesha nia ya kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo ya usafirishaji na usambazaji umeme na
kubwa zaidi katika hili, wameamua kuweka kipengele cha nishati safi ya kupikia kwenye mipango
yao, na hii ni katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania
wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema
AfDB imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo mradi wa umeme wa
Kakono wa megawati 87.8 kwa kuchangia
kiasi cha Dola za Marekani milioni 161 na mradi wa Malagarasi wa megawati 49.5
kwa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 120.
Amefafanua
kuwa, Benki hiyo pia imetoa sehemu ya fedha za utekelezaji wa miradi ya
usafirishaji umeme ukiwemo mradi wa Singida-Arusha-Namanga (kV 400) ambao sasa
umefikia asilimia 99, mradi wa Rusumo-Nyakanazi (94 km) ambao umekamilika kwa
asilimia 100 na mradi wa umeme wa Backbone unaojumuisha ujenzi wa vituo vya
kupoza umeme mkoani Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo kituo cha
Dodoma na Singida vimekamilika kwa asilimia 100.
Kufuatia
hatua hiyo, Dkt.Biteko ameishukuru AfDB kwa kutoa sehemu ya fedha ambazo
zinatekeleza mradi wa usafirishaji umeme wa kV 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma
ambao sasa umefikia asilimia 92.
AfDB pia imeonesha nia ya kufadhili mradi wa usambazaji
wa Gesi Asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam kwa kutumia
mfumo wa ushirikiano na Sekta Binafsi (PPP).
Pia AfDB imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali katika mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ya kV 220 sambamba na kushirikiana na serikali katika uendelezaji miradi mbalimbali ya nishati jadidifu.
Dkt. Biteko amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni fursa adhimu itakayowezesha Taifa kuwa na nishati ya kutosha kwa maendeleo ya nchi.
Kwa
upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kevin Kariuki,
amesema nia ya Benki hiyo ni kuhakikisha
miradi ya umeme inayofadhiliwa na AfDB inakamilika kwa wakati ili kuwapa
wananchi umeme wa uhakika.
Ameongeza
kuwa, Benki hiyo itaendelea kufanya tathmini kuona namna ya kuendeleza mipango
mbalimbali ya Tanzania kwenye gesi asilia ikiwemo kupitia mpango mkakati wa
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili kuainisha maeneo zaidi ya
ushirikiano.
0 Comments