WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inawapenda Watanzania ndiyo maana inatekeleza miradi mingi na kutoa wataalamu katika nyanja zote ili waweze kuwahudumia wananchi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Februari 26, 2024) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa maeneo ya Mariwanda na Sabasita, wilayani Bunda akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Mara.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni imara na ina nia ya dhati ya kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa kufikisha maendeleo kwenye sekta zote za huduma za jamii katika kila eneo nchini.
Serikali ya awamu ya sita inawapenda Watanzania wote ndiyo maana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi mbalimbali ya maeneo katika sekta zote za maendeleo kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa shule ya msingi Sabasita, Mheshimiwa Majaliwa amesema mkakati wa Serikali ni kujenga shule kwenye kila kijiji na kama kuna vitongoji vikubwa au kuna kijiji kina watu wengi, mpango uwe ni kuongeza shule.
Shule hiyo ambayo imejengwa maalum chini ya mpango wa BOOST ili kuwasaidia watoto wa wafugaji wasitembee umbali mrefu kupata elimu, imegharimu sh. milioni 348.2 ambazo zimejenga madarasa tisa yakiwemo saba ya elimu ya msingi na mawili ya elimu ya awali. Kabla shule hiyo haijajengwa, watoto walikuwa wakitembea umbali wa km. tano na sasa umbali huo hauzidi km. moja.
Fedha hizo pia zimetumika kujenga jengo la utawala, matundu ya vyoo 16 ambapo nane ni vya shule ya msingi, sita ni ya awali na mawili ni ya walimu. Ujenzi wa shule hiyo ulianza Mei 16, 2023 na ulikamilika Julai 30, 2023.
Akiwa njiani kuelekea Sabasita, Waziri Mkuu alisimama Mariwanda na kuwasalimia wananchi waliojitokeza njiani kumpokea na kuwaeleza kuwa Serikali inaendelea na uratibu wa mpango wa kuwa na viwanda vya mazao ya mifugo.
“Mifugo ni maisha, mifugo ni uchumi, mifugo ni uwezeshaji wa mtu binafsi ndiyo maana Serikali inawaletea maafisa ugani ili wawasaidie kwenye sekta hiyo. Endeleeni kufuga na mzingatie masharti ya ufugaji ili muweze kukuza uchumi wenu,” amesisitiza.
Waziri Mkuu alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zablon Masatu akae na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Adinani Hamidu ili waangalie uwezekano wa kuongeza vigezo kwenye zahanati ya kijiji kwa kuongeza majengo ya kuhudumia mama na mtoto kutokana na idadi kubwa ya wakazi kwenye kijiji hicho.
Akiwa kata ya Buramba katika jimbo la Mwibara, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Mara ambayo inatarajiwa kugharimu sh. bilioni 4 na itakapokamilika, itachukua wanafunzi wa kike kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Shule ambayo pia itakuwa ya bweni, ilipokea sh. bilioni 3 na hadi sasa imekwishagharimu sh. bilioni 2.82 na kuna bakaa ya sh. milioni 176.7.
Waziri Mkuu aliwasisitiza viongozi wa Halmashauri ya Bunda wasimamie mradi huo na mafundi ujenzi wa shule hiyo wafanye kazi usiku na mchana ili ukamilike mapema na ifikapo Julai, mwaka huu wanafunzi wa kidato cha tano waanze masomo.
Imeandikwa na. Irene Bwire
Imehaririwa na. Prosper Kwigize
0 Comments