Matokeo ya ziara ya Rais Samia nchini Norway haya hapa


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa Hati mbili za Makubaliano na Mkataba mmoja katika ziara yake ya Kitaifa nchini Norway.

Hati ya kwanza imesainiwa na Mhe. Anne Beathe Tvinnereim, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe kwa upande wa Tanzania inayohusu ushirikiano wa Usalama wa Chakula na Kilimo. 

Vile vile, hati ya pili imetiwa saini na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Maisha cha Norway (NMBU) Bw. Siri Fjellheim na Prof. Raphael Tihelwa Chibunda kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Tanzania (SUA)

Pia, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imesaini Mkataba wa Ruzuku Ndogo wa jumla ya Kroner ya Norway Milioni 9.9 sawa na Tshs. Bilioni 2.4 kwa ajili ya kuendeleza Elimu na Utafiti kuhusu masuala ya afya ya udongo na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi 

Hati hiyo imesainiwa na Bw.Ivar H. Kristensen, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi wa Kilimo ya Norway na Dkt. Thomas Nestory, Mkurugenzi Mkuu (TARI).

Wakati huo huo, Rais Samia ametoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuunganisha nguvu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayochangia uhaba wa chakula katika nchi mbalimbali hususan barani Afrika. 

Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa mabadiliko ya Tabianchi na usalama wa Chakula akihitimisha ziara yake ya Kitaifa ya siku mbili nchini Norway.


Hata hivyo Rais Samia amesema pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi, Tanzania kwa mwaka 2022/2023 haijakabiliwa na uhaba wa chakula na imefanikiwa kuziuzia nchi jirani tani milioni tano za chakula ili kukabiliana na tatizo hilo. 

Mbali na kukutana na Mfalme Harald V, Rais Samia pia ameshiriki Mkutano wa Jukwaa la Nishati la Oslo, amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Norway na pia kukutana na Diaspora kabla ya kuhitimisha ziara yake.

Post a Comment

0 Comments