Rais Samia amuaga Lowasa, ahimiza kumuenzi kwa vitendo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Watanzania tuna wajibu wa kuendelea kustahimiliana na kufanya siasa za kistaarabu zinazoweka mbele maslahi ya nchi. 

 

Rais Samia amesema hayo wakati wa ibada ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Ngoyai Lowassa yaliyofanyika katika kijiji cha Ngarash wilayani Monduli.

 

Aidha, Rais Samia amesema njia pekee ya kumuenzi Hayati Lowassa ni kuendesha siasa kwa kuheshimiana, kustahamiliana ili kuleta maendeleo bila kutikisa misingi ya utaifa na mshikamano wetu licha ya kutofautiana mitazamo, misimamo na sera.

 

Vile vile, Rais Samia amesema Hayati Lowassa alikuwa muumini wa elimu kama nyenzo ya kujikomboa na umasikini, hivyo alipenda vijana wapate maarifa na ujuzi kwa ajili ya ustawi wa familia zao na jamii kwa ujumla.

Rais Samia pia amesema katika sekta ya elimu, Hayati Lowassa alisimamia kwa mafanikio Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) akiwa Waziri Mkuu kwa kuratibu na kusimamia ujenzi wa shule za Sekondari katika kila Kata nchini.

 

Hali kadhalika, Rais Samia amesema tangu wakati huo serikali imeendelea kusimamia ujenzi na uendelezaji wa shule za Kata kote nchini, na hivyo kuongeza shule za Serikali kutoka 828 mwaka 2004 hadi shule 4,578 mwaka 2023.



Kwa kutambua umuhimu wa elimu yenye kukidhi mahitaji ya soko la ajira mwaka 2023 serikali imefanya mabadiliko ya Sera na Mitaala ya Elimu ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia.

 

Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Taifa limepoteza moja ya viongozi mahiri, mpenda maendeleo, mwanamageuzi na kipenzi cha wengi.

Post a Comment

0 Comments