Serikali imesema kuwa Tume ya
Mipango itafanya tafiti mbalimbali kubaini fursa za maendeleo katika miji
ikiwemo Mji wa Tunduma kwa lengo kujua ni jinsi gani mji huu na miji mingine
inaweza kuongeza kasi ya maendeleo na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.
Hayo yamelelezwa na leo Februari
2, 2024 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na
Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalaum, Mhe. Neema Mwandabila, aliyeuliza kuhusu mkakati wa Serikali wa
kufanya utafiti maalum katika Mji wa Tunduma ili kubaini ni namna gani unaweza
kuchangia kukuza uchumi wa nchi.
“Tume ya Mipango imejipanga
kufanya tafiti mbalimbali na kuratibu tafiti zitakazofanywa na taasisi nyingine
za umma na binafsi kwa lengo la kubaini fursa za maendeleo katika maeneo
mbalimbali nchini. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Mipango, hususani
kifungu cha 6(2), pamoja na majukumu mengine, Tume ya Mipango ina jukumu la
kufanya utafiti kuhusu suala lolote ambalo Tume inaona ni muhimu katika kufikia
malengo ya maendeleo ya Taifa”, ameeleza Prof. Mkumbo.
Vilevile, Prof. Mkumbo amejibu
swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe. Angelina Mabula kuhusu
utekelezaji wa mradi wa kongano la viwanda lenye ekari 52 lilotengwa katika
Manispaa ya Ilemela eneo la Nyamanoro.
Ambapo, Prof. Mkumbo amesema “Eneo hilo limeshakabidhiwa katika
Taasisi ya EPZA na linafanyiwa kazi, aidha litawasilishwa katika
Bodi na baada ya hapo litatolewa maelekezo maalumu ni lini hasa
ratiba itatoka ya utekelezaji na katika Bunge lijalo tutaeleza Mpango maalumu
kuhusu kongano hilo”.
Mwandishi: Immaculate Makilika
Mhariri: Prosper Kwigize
0 Comments