Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema haki,
demokrasia, sheria na utawala bora utadumishwa kwa watu wote wakati wa Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Rais
Samia amesema hayo leo katika sherehe za mwaka mpya 2024 (Diplomatic Sherry
Party) kwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wawakilishi
wa mashirika ya kimataifa zilizofanyika Ikulu.
Aidha,
Rais Samia amesema ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, Kikosi Kazi huru
cha kupitia na kushauri mageuzi muhimu katika mfumo wa siasa kiliundwa ambapo kiliwasilisha
ripoti yake mwaka 2023.
Rais
Samia pia amesema mapendekezo mengi ya Kikosi Kazi yaliyopokelewa na serikali
na wadau wote yalihusu kuongeza uwazi katika michakato ya uchaguzi ikiwa ni
pamoja na uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.
Vile vile, Rais
Samia amesema masuala machache hayakupokelewa moja kwa moja ambayo
yalikuwa kinyume na katiba hivyo yanaweza kuchukuliwa wakati wa mchakato wa
marekebisho ya katiba.
Rais Samia amesema serikali itaendeleza ushirikiano na
balozi hizo kwa mujibu wa katiba, tunu za
kitaifa, usawa, umoja na mshikamano wa kitaifa huku akiwataka mabalozi hao kutokuingilia uchaguzi na kuzingatia
mila, kanuni na maadili ya
kidiplomasia.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Tanzania inasikitishwa na vita
vinavyoendelea Palestina na kusababisha mauaji ya watoto na raia wasio na hatia
na inaunga mkono usuluhishi kati ya Palestina na Israeli kwa kutoa wito wa
kusitishwa mapigano na kupatiwa misaada ya kibinadamu.
0 Comments