UDOM kuleta mapinduzi katika elimu ya Sayansi na Hisabati


Wakati Tanzania ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu na wasomi wa fani ya Sayansi, Hisabati, Chuo kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia leo wamezindua mpango mahususi wa kujenga uwezo wa walimu kufundisha masomo hayo katika shule za sekondari nchini

Mpango huo unaofadhiliwa na serikali ya Canada kupitia UNICEF unalenga kujengea uwezo walimu 1400 kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora na Songwe na uzinduzi wake unafanyika mjini Kasulu

Ili kufanikisha azima hiyo, Shirika la umoja wa mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF Limefadhili kiasi cha shilingi Bilioni 1.2 kwa serikali ya Tanzania kupitia chuo kikuu cha Dodoma kwa ajili ya kufanya mageuzi katika mfumo wake wa elimu

Hayo yamebainishwa na Dkt. Abdallah Jacob Seni Rasi wa Ndaki ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakati wa uzinduzi wa mafunzo maalumu ya kujengea uwezo walimu wa hesabu na sayansi mjini Kasulu mkoani Kigoma

Dkt. Seni Amebainisha kuwa msaada wa Canada kupitia UNICEF utaleta mageuzi makubwa katika elimu ya Tanzania hasa kwa kuchochea ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati ili kuongeza wataalamu, walimu na wabobevu katika fani za kisayansi nchini

Kwa upande mwakilishi wa UNICEF mkoani Kigoma Bi. Farida Sebarua wakati akihutubia washiriki wa mafunzo hayo amebainisha kuwa  mchango wa UNICEF umelenga kusaidia usawa wa kijinsia katika elimu hasa kuhamasisha ufundishaji wa masomo sayansi kwa watoto wa kike walioko shule za sekondari katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Songwe.

Bi. Sebarua amebainisha kuwa UNICEF kupitia uwezeshaji wa Serikali ya Canada itawajengea uwezo walimu Pamoja na kuboresha miundombinu ya shule hususani ujenzi wa Maabara na upatikanaji wa zana za kisasa za kufundishia na kujifunzia kwa vitendo

Bi. Farida Sebarua mwakilishi wa UNICEF mkoani Kigoma

UNICEF hatufurahishwi na mwenendo wa ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi katika masomo ya Sayansi na Hisabati Pamoja na TEHAMA ndiyo maana tumeamua kuunga mkono juhudi za serikali zinazotambua kuwa ni mhimu kwa wasichana kuhamasishwa kusoma masomo ya sayansi na kuhakikisha jamii pia inaunga mkono mikakati ya serikali na wadau katika mpango huu” Alisisitiza Farida Sebarua.

Akihutubia katika uzinduzi wa mafunzo hayo kwa walimu wapatao 1400, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma idara ya Taaluma, utafiti na huduma za jamii Profesa Razack Lokina amebainisha kuwa taifa la Tanzania limekuwa katika mbinyo wa ukosefu wa wataalamu wa kutosha katika kada ya sanyansi, Hisabati na teknolojia ya habari na mawasiliano hususani kwa wanawake jambo linalorudidha nyuma juhudi za nchi za kukuza Uchumi kupitia sayansi na teknolojia.

Profesa Razack Lokina akihutubia walimu wa sayansi kutoka mikoa ya Tabora na Kigoma katika katika chuo cha Walimu Kasulu mkoani Kigoma  

Prof. Lokina amebainisha kuwa, utafiti uliofanywa na Chuo hicho nchini ulibaini kuwa kidadi ya wasichana/walimu wa kike waliokuwa na ujuzi stahiki wa masomo hayo katika shule za sekondari katika Mikoa ya Kigoma, Tabora na Songwe walikuwa ni wachache kabisa na ufaulu ulikuwa wa chini sana.

Amesisitiza kuwa ili kwenda sambamba na mabadiliko na marekebisho ya mitaala ya elimu nchini Tanzania vyuo vikuu pia vimeanza kipitia mitaala yake ili iendane na ile inayotolewa na shule za sekondari ili wanafunzi watakaoingia vyuo vikuu wawe na mwendelezo mzuri katika masomo ya sayansi hasa wasichana

https://twitter.com/buhafm/status/1759603469067886660   

Hata hivyo hatua hiyo inachambuliwa na wanaharakati kama njia isiyosahihi kutokana na mfumo wa elimu wa Tanzania kutokuwa na misingi thabiti kutoka elimu ya awali na mitaala kutoaandaa walimu na wanafunzi kujali hesabu na hisabati

Kwa upande mwingine wazazi wanalaumu shule za vijijini kutokùwa na walimu wa kutosha au kutokuwepo kabisa na walimu wa masomo hayo.

Hata hivyo Walimu wa masomo ya sanyansi wanajitetea wakidai kuwa mitazamo ya kijamii kuhusu masomo ya hesabu na sayansi kuwa magumu ndiyo chanzo cha Watoto wengi hasa wa kike kuyapa kisogo masomo hayo na kusababisha ombwe la kitaifa

Mwalimu Said Bashira kutoka Kasulu anaeleza kuwa endapo jamii itauondoa mtazamo hasi basi Watoto wengi watayapenda masomo hayo ingawa amekiri kuwa walimu wengi wa masomo ya sanyansi wanahitaji mafunzo kwa kina kutokana na kwamba wengi wao waliyasoma bila kufanya vitendo kwa kiwango kinachotakiwa.


 Mwandishi: Prosper Kwigize

Mhariri: Adela Madyane

  

Post a Comment

0 Comments