"Wagaratia" waonywa kunyemelea jimbo la Profesa Ndalichako

Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Bw. Mbelwa Abdallah amewataka wanaojipitisha kufanya kampeni za ubunge katika jimbo la Kasulu mjini kumwacha profesa Joyce Ndalichako aendelee kuwafanyia kazi wananchi

Bw. Mbelwa ametoa kauli hiyo jana wakati wa halfla ya kupokea magari mawili ya idara ya afya yaliyokabidhiwa kwa viongozi wa wa halmashauri ya mji wa Kasulu pamoja na vifaa tiba na nyezo za kusaidia watu wenye ulemavu.

Akihutubia hadhara iliyofurika katika kituo cha Afya Kiganambo Mbelwa ametaja kuwa kama kuna kitu ambacho wana siasa wanapaswa kuwa na subira nacho ni kuanza kumsumbua mbunge Ndalichako ambaye kazi zake zinaonekana dhahiri ukilinganisha na wabunge wengine waliomtangulia.

"Kuna wagaratia hapa Kasulu ambao sijui nani kawaroga, hawaoni kabisa matokeo chanya ya kazi anazofanya mbunge wetu, wanajipitishapitisha na kumchafua, Mimi nawaambia hakuna aliyefanyakazi nzuri kama huyu mama, natambua kila mbunge alifanya kwa sehemu yake lakini Profesa Ndalichako amefanya zaidi tena kwa kipindi kifupi sana" Alisisitiza Mwenyekiti wa CCM

Profesa Joyce Ndalichako akihutubia wananchi wa mjini Kasulu kabla ya kukabidhi magari na vifaa tiba katika kituo cha Afya Kiganamo mjini Kasulu


Kwa upande wake mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (mkoa wa Kigoma) Bi. Agripina Zaituni Buyogera amemtaja profesa Ndalichako kama mwanamke shupavuu na mwenye kufanyakazi kwa vitendo na mvumilivu.

Bi. Buyogera ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa na aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Kasulu vijijinii kwa tiketi ya Chama cha NCCR Mageuzi anakiri kuwa Profesa Ndalichako amekuwa mbunge wa aina yake na kazi zake hazipaswi kubezwa na mwanasiasa yeyote makini.

Baadhi ya Viongozi wa CCM walioshiriki katika hafla ya kukabidhi magari, vifaa tiba na misaada kwa watu wenye ulimavu kutoka kwa Mbunge Joyce Ndalichako

Miongoni mwa sifa anazopewa Profesa Ndalichako ni pamoja na kasi yake ya kusaidia miradi ya maendeleo katika sekta zote hususani elimu, afya, maji na huduma za jamii

Miradi mikubwa aliyosimamia ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, ukarabati wa hospitali, ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, vyuo vya ufundi na chuo cha ualimu Kabanga, Veta Nyumbigwa, shule maalumu ya watu wenye ulemavu Nyumbigwa, ujenzi wa barabara mpya za lami mjini na huduma kwa watu wenye ulemavu bila ubaguzi.

Profesa Ndalichako akimsaidia mama mwenye Ulemavu ambaye amekabishiwa kitimwendo kipya kwa ajili ya kusaidia harakati zake za maisha ya ulemavu, huku akionesha tabasamu la matumaini mapya ya maisha

Watu wanaotajwa kuwa ni "wagaratia" ni waliowahi kuwa wabunge wa jimbo hilo ambao wamebainika
kuendelea kufanya vikao vya siri na ziara za kisiasa katika kata mbalimbali wakimchafua profesa Ndalichako ili wao waaminiwe hata katika kipindi ambacho si cha uchaguzi wala kampeni.

Chama Cha Mapinduzi wilayani Kasulu kupitia kwa mwenyekiti wao Mbelwa Abdallah Chidebwe kimejiapiza kuwafuatilia na kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama hicho.

Post a Comment

0 Comments