Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amezindua mradi mkubwa wa umeme Jua
utakaozalisha megawati 150 katika Kijiji cha Ngunga wilayani Kishapu Mkoa wa
Shinyanga ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuibua, kuendeleza na
kutekeleza vyanzo mbalimbali vya umeme ili kuondokana na utegemezi wa Maji na
Gesi Asilia kuzalisha umeme.
Dkt. Biteko amesema mradi huo utaanza kuzalisha megawati 50 ifikapo mwezi
Januari mwaka 2025 na hii ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan la kuongeza vyanzo vya umeme kwani vilivyopo bado havitoshelezi mahitaji.
“ Vyanzo vingine vya umeme tunavyoviendeleza ni pamoja na mradi wa Jotoardhi Songwe na Mbeya ambapo tarehe 1 Aprili mwaka huu uchorongaji unaanza katika eneo la Ngozi, mradi mwingine unaoenda kutekelezwa ni mradi wa megawati 100 wa upepo uliopo Makambako ambapo fidia imeanza kulipwa.” Amesema Dkt. Biteko
Ameeleza kuwa kutekelezwa kwa mradi huo mkoani
Shinyanga, kunafanya Mkoa huo kuwa kitovu cha umeme katika Ukanda wa Ziwa kwani
mpaka sasa kuna vituo vikubwa vitatu vya umeme ambavyo ni Ibadakuli, Bulyanhulu
na Buzwagi ambavyo vinasambaza umeme kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Aidha amesema kuwa, kituo cha Ibadakuli
kinaimarishwa ili kiwe kikubwa zaidi na
hivyo kuweza kusambaza umeme ndani na nje ya nchi kupitia makubaliano ya
ushirikiano katika Sekta ya umeme kwa nchi za
Mashariki mwa Afrika ambapo
itajengwa laini kubwa ya msongo wa kV 400 kutoka Ibadakuli hadi Masaka Uganda
ili kuunganisha Tanzania na Uganda kupitia Kagera.
Kuhusu usambazaji umeme vijijini Mkoa wa
Shinyanga amesema kuwa, mkoa huo una Vijiji
509 ambapo vijiji 127 bado havijapata umeme.
Kufuatia hali hiyo, Dkt. Biteko amewataka
wakandarasi ambao wamechelewa kufikia
lengo la usambazaji umeme kwenye mkoa huo kampuni ya Suma JKT na Tontan
kuhakikisha kuwa wanamaliza kazi husika kwani uzembe kwenye miradi hiyo haukubaliki.
Vilevile, ameziagiza TANESCO na REA kuhakikisha
kuwa wanawapelekea wananchi umeme kwa haraka na kama kuna changamoto ya umeme
wananchi hao wapate taarifa mapema.
Aidha Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa
Serikali kuhakikisha kuwa wanaweka mitambo ya umeme Jua kwenye majengo yao ili
kutokuwa tegemezi kwenye umeme wa gridi pekee na kusema kuwa Wizara ya Nishati
na Taasisi zake zitaanza kutekeleza suala hilo.
Pia ameishukuru Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kutoa fedha za
kutekeleza mradi huo kwa awamu ya kwanza (50 MW) shilingi bilioni 118.677
na kutenga shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya
mradi wa megawati 100.
Awali, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Costa Rubagumya alisema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ikiwa ni megawati 50 na awamu ya Pili itazalisha megawati 100 huku eneo la mradi likiwa ni hekta 570.
Aliongeza kuwa, Awamu ya kwanza ya mradi ya megawati 50 itagharimu jumla ya
shilingi bilioni 118.677 huku awamu ya pili ikigharimu shilingi bilioni
204.419 na kufanya mradi mzima kugharimu shilingi bilioni 323.096.
Ameeleza kuwa, fedha za utekelezaji wa mradi zimetoka Shirika la Maendeleo la
Ufaransa ( AFD) kwa kiasi cha shilingi bilioni 320.255 huku Serikali ya
Tanzania ikitoa shilingi bilioni 2.841 ambazo zimetumika kama fidia kwa
wananchi waliopisha maeneo.
Ameongez
kuwa, awamu ya kwanza ya mradi inatekelezwa na Mkandarasi Sinohydro kutoka China na mradi
utakamilika Januari 2025 ambapo awamu ya Pili ya utekelezaji mradi itaanza
Agosti 2024 na itachukua miezi 12 kukamilika.
Kwa upande, Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo ameeleza kuwa mradi huo
licha ya kuongeza kiwango cha umeme kwenye gridi ya Taifa na kuboresha hali ya
umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini, Halmashauri ya Kishapu itafaidika
na ushuru wa huduma utakaolipwa kutokana na mradi kuwepo kwenye eneo hilo.
Ameongeza kuwa kutokana na uwepo wa mradi, Halmashauri ya Kishapu imeshaanza
kuona matunda yake kwani wameshapata shilingi milioni 600 kutokana na sera ya
uwajibikaji wa kampuni kwa jamii ( CSR) ambazo zitatumika katika masuala
ya Afya, Barabara, Maji, Shule n.k
0 Comments