Naibu Waziri, ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Patrobas Katambi ameeleza kuwa maandalizi ya uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru yamekamlika kwa zaidi ya asilimia 90 huku akihimiza mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha unahamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika tukio hilo la hilo la kihistoria.
Ameyasema hayo wakati akikagua maandalizi ya uzinduzi wa mbio hizo katika uwanja wa michezo wa chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCU), mkoani Kilimanjaro.
Amesema kuwa Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2024 zinaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa rasmi mwaka 1964 zikienda sanjari na miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Rajab amesema kuwa ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara hiyo wamekua wakishirikiana kwa karibu na ofisi ya mkuu wa mkoa huo wa Kilimanjaro katika kuhakikisha maandalizi yanakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Kwa upande wake, kaimu katibu Tawala mkoa wa Kilimanjaro,Jackson Masaka amesema viongozi wa mkoa wamekua na utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi ikiwemo Bodaboda, Wazee, Wafanyabiashara, Wanawake kwa lengo la kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2024 zinaogozwa na kauli mbiu isemayo “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.
Mwandishi:Na: Mwandishi Wetu
Mhariri: Adela Madyane
0 Comments