Prof. Ndalichako azindua wiki ya maji Kasulu

  • Azindua mradi wa maji uliokwama kwa zaidi ya miaka 30 kutokana na hujuma
  • Ampongeza rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo

Mbunge wa jimbo la Kasulu mjini Profesa Joyce Ndalichako leo amezindua mradi wa maji wa uliokuwa umesimama kwa miaka 30 iliyopita kutokana na kuhujumiwa kwa miundombinu

Uzinduzi huo umefanyika katika mtaa wa Nyachijima kata ya Kigondo wilayani Kasulu ikiwa ni sehemu ya sherehe za wiki ya maji ambayo huadhimishwa duniani kila mwaka ifikapo March 16 hadi 22

Akihutubia wananchi walioshuhudia uzinduzi huo, Profesa Ndalichako amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha nyingi za maendeleo hususani miradi ya maji

Amebainisha kuwa mpango wa serikali ni kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa kutambua kuwa huduma ya uhakika ya maji kwa amani na utulivu kama ilivyo kauli mbiu ya wiki ya maji duniani.

“Sisi wana Kasulu tuna kila sababu ya kumshukuru rais wetu mpendwa Dr. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kutekeleza miradi yam aji ili kuhakikisha anatupatia amani na utulivu” amesisitiza Prof. Ndalichako

Prof. Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji Nyachijima mjini Kasulu uliokuwa umetelekezwa kwa zaidi ya miaka 30. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kigoma Zaituni Buyogera na kulia kwake ni Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu

Amebainisha kuwa ipo miradi mingine ukiwemo mradi mkubwa wa mto Ruchugi ambao serikali imetoa kiasi cha sh. Bilioni 35 pamoja na mradi wa kabanga wa chujio la maji na mradi wa Mwanga ambao utasambaza maji katika vijiji vingi ikiwemo Mwanga, Mganza na kabanga

Prosfesa Ndalichako ameweka bayana kuwa Mji wa Kasulu ulikuwa na asilimia 60 ya kiwango cha upatikanaji wa maji ukilinganisha na maeneo mengine ambapo ni zaidi ya asilimia 80, na kusisitiza kuwa kutokana na miradi inayoendelea Kasulu itafikia asilimia 95 ya upatikanani wa maji kwa uhakika ifikapo 2025.

Ametaja kuwa ipo miradi mingi ya Maji inayotekelezwa katika jimbo la ka Kasulu mjini ikiwemo ya Mdyanda na Nyantale ambayo inawatua ndoo kichwani akina mama na kuwapunguzia adha ya kutafuta maji kutoka umbali mrefu ikiwemo nyakati za usiku ambako usalama unakuwa mdogo.

Prof. Ndalichako akimtwisha ndoo ya Maji Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu wakati wa uzinduzi wa mradi huo 

Hata hivyo Prof. Ndalichako amekiri kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya mitaa kupata maji machafu bombani na kutaja kuwa tayari serikali kupitia katika ushawishi wake imeanza utekelezaji wa mradi wa chujio katika chanzo cha Mto Chai ambao utaondoa kero ya mabomba kutoa maji machafu.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa maradi wa maji wa Nyachijima, Kaimu Meneja wa mamlaka ya maji mjini Kasulu Mhandisi Jeremiah Lema ametaja kuwa ufufuaji wa mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 30.7 ikiwemo ujenzi wa mifumo ya usambazaji kwa umma kupitia katika vituo vinne vya uchotaji maji.

Prof. Ndalichako akimsisitiza Kaimu Meneja wa mamlaka ya Maji mjini Kasulu Mhandisi Jeremiah Lema kuhakikisha maji yanapatikana muda wote katika mradi huo na si kufanya maigizo ya uzinduzi

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu amewataka wananchi pamoja na kufurahia huduma za zinazoletwa na serikali watimize wajibu wao wa kutunza mazingira na vyanzo vya maji ili huduma hiyo iwe endelevu

Aidha kanali Mwakisu amewataka watumiaji wa maji wote kuhakikisha wanalipa Ankara za maji kila mwezi kwa mamlaka ya maji mjini Kasulu ili kuipa fursa serikali kufanya matengenezo na kuboresha huduma kwa umma.


 

  

Post a Comment

0 Comments