REA yatimiza ahadi ya kuboresha miundombinu Chekelei


Walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Chekelei iliyopo kijiji cha Madumu, wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga wameishukuru serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuhakikisha wanapata huduma za msingi kwa lengo la kuboresha taaluma shuleni hapo.

Akitoa shukrani hizo Mkuu wa shule, Siwema Mashoto amesema miongoni mwa huduma za msingi walizopatiwa ni pomoja na umeme, makaratasi, mashine ya printa na wino.

Viongozi wa Shule ya Sekondari Chekelei iliyopo Kijiji cha Madumu wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga wakipokea Vifaa mbalimbali ikiwemo  kutoka kwa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ikiwa ni ahadi ya Serikali kuwezesha matumizi ya umeme yenye tija kwa wananchi vijijini

Amesema wanaishukuru Bodi ya Nishati Vijijini (REB) na menejimenti ya REA kwa kutimiza ahadi iliyotolewa Machi mwaka jana ya kuboresha miundombinu ya shuleni hapo na aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

“Tutafanya mabadiliko katika kiwango cha taaluma, tutahakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka ili kuonesha tofauti kabla ya na baada ya kupatikana kwa huduma hizi”Amesema Mashoto

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa REB Jacob Kingu amewataka walimu na wanafunzi kutunza vyema vifaa walivyopatiwa na kuvitumia kwa tija ili vilete manufaa yanayokusudiwa kwao.


Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu akizungumza wakati wa tukio la Bodi na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA),la kukabidhi vifaa shuleni Chekelei 

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye pia ni Katibu wa Bodi,Hassan Saidy amesema wanatamani kuona wananchi wote waliofikiwa na umeme wanautumia kwa tija ili azma ya serikali inayolenga kuboresha maisha vijijini itimie.

“Tunataka wananchi waelewe kwamba kuunganisha umeme peke yake haitoshi ikiwa hautumiki kubadili maisha. Printa na vifaa vingine tulivyowapatia leo, vinalenga kuleta tija ya uwepo wa umeme shuleni hapa,” amefafanua mkurugenzi mkuu.

Vile vile Mkurugenzi huyo ametoa ahadi kuwa REA itawapatia majiko banifu walimu wote wa shule hiyo pamoja na viongozi mbalimbali ili wawe mabalozi wazuri wa ajenda ya Rais Samia ya kumtua Mama kuni kichwani kwa kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Katibu wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Hassan Saidy akizungumza wakati wa tukio la Bodi hiyo na Menejimenti ya REA, kukabidhi vifaa mbalimbali ikiwemo Printa ya kisasa kwa Shule ya Sekondari Chekelei 

Pia, ameahidi kuwa REA itakamilisha kazi ya kutandaza mfumo wa nyaya za umeme katika majengo yote ya shule hiyo ili umeme ambao umekwishafikishwa utumike kwa tija zaidi

Akizungumza Katibu wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM) wa kata ya Chekelei, Mohamedi Fumbili ameipongeza kwa kutimiza ahadi akinukuu maneno kutoka Vitabu vitakatifu kuwa ‘anayeahidi na kutimiza anapata thawabu kwa Mungu.”

Aidha ameongeza kuwa tukio lililofanywa na REA ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na hivyo kumuheshimisha Mwenyekiti wake, Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali kwa ujumla.

Bodi ya Nishati Vijijini iko mkoani Tanga kushiriki vikao vya kazi na hivyo inatumia fursa hiyo pia kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini.

Mwandishi:Na Veronica Simba

Mhariri: Adela Madyane

Post a Comment

0 Comments