Tabata wakataa baadhi ya majina ya mitaa, limo la Msolla


WAKAZI wa eneo la Tabata Mtambani Jijini Dar es Salaam wamekataa majina ya viunga viwili vya Mtaa huo "Kilimani" na "Msolwa" yaliyotokana na  mpango wa anuani za makazi (post code). 

Badala ya Kilimani, wakazi hao wanataka jina Aroma lirasimishwe kutambulisha kiunga hicho na Msolwa likitakiwa kupisha jina la mmoja kati ya waliokuwa wakazi wawili wa kiunga husika, ambao wote kwasasa ni marehemu. 

Hayo yameibuka kupitia mkutano wa hadhara uliyoitishwa na Mjumbe wa Shina Namba Kumi, Johnson Mulima, chini ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtambani, Brigitte Nchimbi, kwa nyakati tofauti wananchi hao wameeleza kero zao na baadhi zikapatiwa ufumbuzi. 

Kuhusu kero ya majina, Mulima amesema kama ilivyo kwa wananchi, hata yeye alikuta vibao vya majina vimesimikwa, hivyo wanaomtuhumu kuhongwa fedha ili majina hayo yatumike kutambulisha maeneo yao, wanamkosea. 

Hata mimi nasikia Msolwa ni kiongozi wa timu ya mpira wa miguu ya Yanga, anaishi wapi huko sijui... na Kilimani wanasema linatokana na guest house (Nyumba ya wageni) ya hapa mtaani," amesema Mulima. 

Baada ya kusikiliza kero za wananchi hao, Nchimbi amekiri kutoshirikisha wakazi hao wala Mulima katika mchakato wa kupata majina hayo na kuyaweka kwenye viunga husika. 

Lakini anamlaumu Mulima kuwa ndiye chanzo cha hayo, kwamba licha ya mara kadhaa kutakiwa apeleke majina yaliyopitishwa na wakazi wa shina hilo, hakutoa ushirikiano. 

"Wajumbe wote katika mtaa wetu walileta majina isipokuwa huyu kiongozi wenu, mpaka nikalazimika kutafuta yeyote aliyekuwa tayari kugharamia nguzo na kuandika jina kwenye kibao, nikapata hao sasa ningefanyaje?" amehoji Nchimbi. 

Hata hivyo kibao chenye jina la “Kilimani” kilichosimikwa jirani na Jengo la Aroma kimeishang’olewa na wasiojulikana.  

Nchimbi amesema kibao hicho kitarudishwa na kiking'olewa tena washukiwa wa kitendo hicho akiwemo Mulima, watachukuliwa hatua za kisheria. 

Baadhi ya wakazi wa Tabata wakiwa kwenye kikaoo cha mtaa kilichoibua hoja ya kuyatakataa baadhi ya majina ya mitaa yao. Picha zote na Editha Majura

Kwa nyakati tofauti wakazi hao wakamhakikishia Nchimbi kuwa hawatakubali eneo la makazi yao kutambulishwa kwa jina hilo, kwamba kwa umoja wao wapo tayari kulipa gharama ili liandikwe jina wanalopenda. 

Akaawabembeleza akisema, uhakiki wa majina ya viunga vya mitaa pamoja na namba za kwenye nyumba utaanza karibuni, wakubali kirudishwe mpaka uhakiki upite, jambo ambalo wakazi hao wamelikataa katu. 

Kwa upande wa jina la “Msolla” wakazi wa kiunga hicho kwa nyakati tofauti wamesema wanapendekeza kitambulishwe kwa jina la mzee Komba au Kombani (marehemu).

Zamani ilikuwa Mtu akipita kwenye hiki kibarabara anaonekana kichwa tu, mwili upo korongoni na wengi tulivunjika miguu kwa kuanguka kutokana na ubovu wake lakini mzee Komba, alimwaga vifusi kisha akamimina zege kwa gharama zake binafsi," anasema Anna na kuendelea 

"Mpaka sasa kila mkazi wa hapa, hata hao waliotuletea hilo jina wanafahamu kuwa tunapita njia hii kwa raha kutokana na wema wa huyu mzee, sasa kwanini tusimuenzi?  Kama huyo hawamtaki wangemuweka mzee Kombani, maana ndiye mwenyeji kuliko wengine wengi hapa."

Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Mtambani, Maria Samweli, ameombwa kuzungumzia hilo akasema wasing’oe vibao hivyo badala yake wawasilishe malalamiko yao ofisini kwake ili yashughulikiwe kwa taratibu sahihi.

Mwandishi: Editha Majura, Dar es Salaam

Mhariri: Adela Madyane

Post a Comment

0 Comments