Vyeo visiwe sababu ya kiburi na majivuno kwa watendaji -Biteko


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati kuanzisha Kitengo maalum cha usimamizi wa Nishati Safi ya Kupikia ili kutekeleza kwa ufanisi ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia na siyo tu kuishia kwenye kuandaa na kushiriki makongamano kisha masuala yote yanaishia hapo.

Amesema hayo tarehe 18 Machi, 2024 jijini Mwanza wakati akifungua Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara  ya Nishati wenye lengo mahsusi la kupitia na kupitisha rasimu ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/2025.

 “Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye kinara wa utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia Afrika hivyo wizara lazima iweke mkakati wa kitaasisi na kimfumo ili kufanikisha ajenda hiyo ili utekelezaji wa suala hili usiwe ni jambo la zimamoto.” Amesema Dkt. Biteko

Vilevile, Dkt.Biteko amesema kuwa, Wizara ya Nishati ina jukumu la kuihamisha nchi kutoka matumizi ya mafuta na kuhamia kwenye matumizi ya gesi (CNG) kwa kutengeneza mazingira ambayo yatapunguza utegemezi wa mafuta na hivyo kufanya nchi kujiendesha kwa kutumia CNG, kutokana na hilo, ameagiza Watendaji wa Wizara kusimamia pia utekelezaji wa suala hilo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto  Biteko (katikati), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (Wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa (wa tatu kutoka kulia) wakiimba wimbo wa Wafanyakazi wa Mshikamano wakati Mhe. Dkt. Doto Biteko alipofungua Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara  ya Nishati tarehe 18 Machi 2024 jijini Mwanza.

Kuhusu Watumishi wa Wizara ya Nishati, Dkt. Biteko  amewakumbusha Watumishi kufanya kazi kwa bidii huku wizara ikiangalia stahiki zao ikiwemo motisha.

Amesema kuwa, Watumishi wa Wizara ya Nishati wana deni la kuwatumikia Watanzania kwani ndio waliopewa dhamana ya kusimamia Sekta ya Nishati kwa niaba yao hivyo watimize wajibu huo.

Vilevile, ametoa wito kwa  Wizara ya Nishati kuwa na utaratibu wa kuwapa motisha watumishi wanaofanya vizuri katika kazi na wale wazembe na wasiotumikia wananchi kwa weledi na kwa wakati watambuliwe pia na kuchukuliwa hatua stahiki.

Aidha, ametoa angalizo kwa wenye mamlaka ndani ya Wizara na Taasisi zake kutoona fahari ya kutumia vyeo vyao kwa ajili ya kuabudiwa na kutukuzwa kwani nafasi walizonazo ni za muda tu, hivyo wajijengee marafiki zaidi kuliko maadui na kujikita katika kuhudumia wananchi na hivyo kuepuka kuchafua utendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake.

Pia, amewataka Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati kupitia bajeti hiyo kwa umakini kabla haijafika katika ngazi ya Kamati ya Bunge na baadaye  katika Bunge la Bajeti.

Watendaji wa Wizara ya Nishati wakiwa katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara  ya Nishati ambao umefanyika tarehe 18 Machi 2024 jijini Mwanza.

Ameongeza kuwa, kama kuna changamoto zozote ambazo Baraza hilo wanaona kuwa zipo katika Sekta basi wazijadili na kutoa njia mbadala ya kutatua changamoto hizo.

“Mfano, pamoja na mradi wa Julius Nyerere kuanza kuzalisha umeme lakini bado tunapaswa kuendeleza miradi mingine kwani JNHPP ni holiday ya muda mfupi, kama tunafikiria miaka 50 mbele lazima tutambue kuwa lazima tuendeleze vyanzo vingine vya umeme ili kuwa na umeme wa ziada.” Amesema Dkt. Biteko

Awali Mwenyekiti wa Baraza ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema kuwa baada ya Baraza hilo kupitisha Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2024/ 2025 hatua inayofuata ni kupitishwa kwenye Kamati za Bunge na baadaye Waziri wa Nishati ataisoma bungeni kwa ajili ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuhusu bajeti ya mwaka 2023/2024, Mhandisi Mramba amesema kuwa masuala yaliyopangwa kufanyika kwenye bajeti hiyo yametekelezwa kwa kiasi kikubwa na hii ikitoa mwanga kuwa bajeti ijayo pia itatekelezwa vizuri.

Ameongeza kuwa, kwa sasa Sekta ya Nishati inatazamwa upya kwa kuangalia mchango wa nishati jadidifu katika Sekta, nishati bora ya kupikia, uhifadhi wa nishati na matumizi bora ya nishati lengo likiwa ni kuiboresha zaidi Sekta husika kwenye nyanja mbalimbali. 

Post a Comment

0 Comments