Wafanyabiashara wanawake Kigoma walia na soko

Wanawake wafanyabiashara wa mazao ya samaki na dagaa mkoani Kigoma wameiomba serikali kuboresha eneo la soko katika mwalo wa Kibirizi kutokana na eneo hilo kujaa maji yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Wakizungumza na Buha News kitengo cha mazingira wiki hii wanawake hao Wamesema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha kujaa maji kwa mwalo huo uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuharibu miundombinu ya soko na kusababisha kuhamishwa kutoka katika eneo hilo na kupelekwa katika maeneo mengine ya soko hali inayokwamisha shughuli za biashara.

Miongoni mwa masoko walikohamishiwa wafanyabiashara hao ni pamoja na eneo la pembenzoni mwa mwalo wa Kibirizi, takribani kilomita mbili kutoka lilipokuwa soko la awali, wengine wamepelekwa katika soko jipya lililoanzishwa maeneo ya machinjio ya Kibirizi pamoja na soko la Gungu.

Akizungumza Mariam Shaban mfanyabiashara wa samaki wabichi amesema kipato chake kimeshuka kutokana na kuhamishwa kutoka eneo la soko ambalo wateja walikuwa wamelizoea na kwamba samaki wamekuwa wakiharibika kutokana na kukaa muda mrefu bila kuuza.

“Nilikuwa nauza zaidi ya elfu 20 kwa siku, ila sasa nauza elfu tatu kwa siku, hali ya maisha yangu imebadilika ghafla, serikali itutengee eneo maalumu la soko linalofikika kwa urahisi, huku ni mbali, wateja hawafiki na mboga zinaharibika, tutawaleaje watoto wetu” amesema Shaban

Eneo jipya la soko walikohamishiwa wafanyabiashara wa samaki na dagaa

Naye Hassan Juma, alisema serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuboresha miundombinu ya soko au kutenga eneo maalumu la soko  kwasababu changamoto ya kujaa kwa maji katika eneo hilo inakwamisha shughuli za biashara na kuathiri upatikanaji wa kipato cha kila siku.

Naye Fatuma Rashid mfanyabiashara katika soko lililopo pembeni mwa mwalo alisema eneo walilopo ni la mtu binafsi jambo ambalo haliwapi uhakika kwani mwenye eneo lake anaweza kubadili mawazo na kutaka kuwaondoa katika eneo hilo na kuwafanya waanze kutangatanga.

Katika nyakati nyingine, wananchi wamelalamikia uharibifu wa miundombinu ya bandari ndogo ya Kibirizi kutokana na kujaa maji hali iliyopelekea kukwama kwa shughuli za kibiashara ndani ya mkoa na nchi jirani.

Msafirishaji wa mizigo na abiria kwenda maeneo ya mwambao mwa ziwa Tanganyika, Issa Mustapha alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na mvu zinazoendelea kunyesha ni muhimu serikali ikaongeza nguvu katika kuboresha bandari hiyo kutokana na kujaa kwa maji katika bandari hiyo kwani wamekuwa wakitegemea kuendesha maisha yao kwa kusafirisha mizigo na abiria.

“Gati limejaa maji na inatulazimu kutembea na mzigo mita kadhaa ukiwa umeubeba ndani ya maji ili kuingiza ndani ya boti hali hii inaweza kusabisha hasara kwa wenye mizigo endapo utadondoka kwenye maji wakati wa kubeba,” alisema Mustapha

Kufuatia malalamiko hayi kaimu ofisa biashara wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Kanyama Kalombo amesema wanaendelea na mchakato wa kuwaandalia wafanyabiashara hao maeneo ya kufanya biashara zao kwa muda ambapo watafanya kwa uhuru na kuendelea kuingiza kipato Chao kama kawaida.


Eneo la soko katika mwalo wa Kibirizi ambalo limejaa maji na kusababisha wafanyabiashara kuhamishwa.

Naye meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Kigoma, Silvester Mabula amesema wanajipanga kufanya tathmini na kuangalia njia mbadala ili wateja wao na wananchi waweze kuendelea kupata huduma za usafiri na usafirishaji kama awali.

“Kutokana na kujaa maji TPA haijakaa kimya inaangalia njia mbada kuhakikisha huduma za wateja zinaendelea kufanyika kama kawaida na tunafanya tathmini ya gharama zinazohitajika kwaajili ya kuangalia upande mwingine wa banadari hiyo kwaajili ya kutengeneza njia nyingine ambayo wataitumia wateja wetu kwani eneo hili ni muhumu sana kwetu,”alisema Mabula

Kwa upande wa mkuu wa wilaya ya Kigoma, Salum Kalli aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuwataka wafanyabiashara wa samaki na dagaa wa eneo hilo kuhama kwa muda kutokana na maji kuongezeka katika eneo lao la biashara.

“Katika wilaya yetu tuna masoko mengi niwaombe muhamie huko kwa muda ili muendelee kufanya biashara zenu na kupaacha wazi hapa ili tuweze kujipanga na kupaboresha zaidi, ili eneo hilo liwe rafiki na maji yakiongezeka kwa wakati mwingine yasiweze kufika eneo hilo,”alisema Kalli

Amesema hakuna sababu ya wafanyabiashara hao kupanga biashara zao barabarani kwani masoko yapo ya kutosha kwa ajili ya wao kufanya biashara, huku akiongeza kuwa wao na wafanyabiashara wanategemea katika kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuendesha familia zao.

Mwandishi: Na mwandishi Wetu

Mhariri: Prosper Kwigize 



Post a Comment

0 Comments