Wakatoliki wahimizwa kuzingatia miongozo ya kanisa na maadili ya jamii

 


Waumini wa Kanisa Katoliki wamehimizwa kuwa na msimamo wa kweli katika Imani yao na kujiungamanisha na Mungu katika wiki hii takatifu kuelekea sikukuu ya Pasaka

Rai hiyo imetolewa wakatii wa Misa ya sikukuu ya Matawi na Padri Danieli Kabuya wa kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Marko mwinjili Kabanga wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma

Akiwahubiri waumini wa kanisa hilo katika misa takatifu ya matawi na wiki ya mwisho wa mwezi wa kwarezima  amesema katika kipindi hiki cha sherehe za waumini wanatakiwa kukua kimwili na kiroho ili kuimarisha Imani zao

Amesema kipini hiki cha juma kuu kila muumini anatakiwa ajitenge na dhambi na kujiweka mbele ya Mungu ili kufanya kitubio na kuachana na Imani potofu zinazo zuka kama vile kamchape au lamba lamba.

Ameeleza kuwa, chanzo cha kuwepo na ongezeko la Imani potofu pamoja na makundi ya kiuhalifu ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili unaosababishwa na malezi mabaya kuanzia ngazi ya familia.

Padre Kabuya ametumia fursa hiyo kuwaasa waumini, wazazi na walezi kuanzia ngazi ya familia kuwajibika ipasavyo kwa kufuatilia nyendo za watoto wao pamoja na makundi ya marafiki wanaocheza nao na kujua kila hatua ya maendeleo yao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kanisa hilo Bw. Alex Phabian amesema katika kipindi cha Jumapili ya matawi tunaalikwa kujitathimini katika maisha ya ukristu na kuangalia kama mienendo inazingatia taratibu za ukatoliki.

Amesema yapo madhara mengi yatokanayo na kuamini ushirikina mojawapo ikiwa ni uvunjifu wa amani na kushuka kwa imani na kusababisha kukosa maelewano miongoni mwa jamii.

Mmomyoko wa maadili ni moja tajwa kuwa chazo kikuu cha ongezeko la vitendo viovu katika jamii na kusababisha ongezeko la Imani potofu na kuongezeka kwa makundi ya uhalifu mtaani ikiwemo wizi

Akizungumza na Buha News kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Bi. Getrude Edward amekiri kuzorota kwa imani katika jamii na kueleza kuwa hatua mbalimbali zinachukuliwa ikiwemo utoaji wa elimu katika ngazi za familia na jumuiya.

Wiki hii waumini wa madhehebu ya kikristo duniani wanaadhimisha Juma kuu linalohusisha Jumapili ya matawi, Alhamisi Kuu, Ijumaa kuu na sikukuu ya pasaka ambayo itasherehekewa April mosi mwaka huu.

Mwandishi: Sara Mataro

Mhariri: Prosper Kwigize

                                                                               

Post a Comment

0 Comments