Watanzania wachangamkia matumizi ya gesi kwenye magari

 

Idadi ya watanzania wanaotumia gesi kwenye magari yao kama mbadala wa Petrol na Dizel imeongezeka na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yanayofanya mageuzi katika kupunguza hewa ukaa dunini 

Hayo yalibainishwa Katika taarifa ya uendeshaji wa vituo vya ujazaji wa Gesi iliyowasilishwa na Mha. Aristides Katto kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na madini ilizuru kituo hicho mapema jana. 

Mhandisi Katto alisema TPDC inatekeleza mpango wa ujenzi wa vituo vitatu vya CNG katika Jiji la Dar Es Salaam pamoja na Mkoa wa Pwani ambapo vitajengwa pembezoni mwa barabara ya Sam Nujoma eneo la Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. 

Amesema kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wateja wanaohitaji kubadilisha magari yao kutoka kutumia mafuta ya dizeli na petroli na kutumia gesi asilia ambayo ina gharama nafuu ikilinganishwa na nishati ya petroli na dizeli. 

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imekagua vituo vya gesi iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas – CNG Stations) katika eneo la Ubungo Maziwa pamoja na Kituo cha Taqa – Dalbit vilivyopo Kipawa jijini Dar es Salaam. 

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imekagua vituo vya gesi iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas – CNG Stations) Kituo cha kujazia gesi kwenye magari cha  Taqa – Dalbit kilichopo Kipawa jijini Dar es Salaam. Wa Saba kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe, David Mathayo  na wa Tano kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. David Mathayo aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya uwekezaji katika sekta ya nishati  kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. 

Alisema, “tunajua Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuhakikisha inawekeza katika sekta hii ambayo itawezesha watanzania wengi kupata nishati ya gesi kwa gharama nafuu na kuepukana  na gharama kubwa za mafuta.” 

Kamati hiyo iliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya gesi katika mikoa mingine nchini ili kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na huduma hiyo ambayo kwa sasa inapatikana katika Jiji la Dar Es Salaam pekee. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga aliahidi kuuzingatia ushauri wa Kamati hiyo ili kuendelea kuleta mapinduzi katika sekta ya nishati. 

Amesema kwa sasa Serikali ina mkakati wa kushirikiana na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuongeza karakana kwa ajili ya kubadilisha mifumo ya nishati katika magari ili wananchi wengi waweze kupata huduma hiyo ya gesi. 

Ziara hiyo imehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC Ndg. Mussa Makame na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TPDC.

Mwandishi: Teresia Mhagama

Mhariri: Prosper Kwigize

Post a Comment

0 Comments