JKCI yabaini matatizo ya moyo Kagera

Mkoa wa Kagera umebainika kuwa na changamoto ya magonjwa ya moyo jambo linaloisukuma taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuweka mkakati mahususi kuisaidia jamii ya Kagera

Watu 34 kati ya 194 waliofanyiwa uchunguzi kwenye kambi maalum ya madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mkoani Kagera sawa na asilimia 17 wamekutwa na matatizo ya moyo.

Takwimu hizo zimetolewa leo Alhamisi Machi 21, 2024,na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka JKCI, Dk Yona Gandye wakati wa kambi ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Bukoba mkoani Kagera kuanzia Machi, 18 mwaka huu.

Dk Gandye amesema waliobainika kuwa na tatizo la moyo lililofika hatua mbaya wamepatiwa rufaa ya kwenda kupatiwa huduma za kibingwa katika taasisi ya JKCI iliyoko mkoani Dar es Salaam.

Awali, Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto JKCI, Dk Nuru Letara ametaja baadhi y tabia zinazochangia watoto kuugua magonjwa ya moyo ikiwemo mjamzito kutomeza dawa za vitamini 'Folic acid' ipasavyo, uvutaji sigara na unywaji wa pombe.

"Nikitolea mfano katika Taasisi ya JKCI pekee tunapokea watoto 30 hadi 40 kwa siku wenye matatizo ya moyo na watoto zaidi ya 300 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika hospitalini hapo," amesema Dk Letara.

Amewataka wazazi kuweka mipango kabla ya kushika ujauzito ili kuhakikisha mtoto anayezaliwa anakuwa na afya njema kwani mtoto mwenye afya ni matokeo ya maandalizi mazuri ya wazazi.

Mkuu wa mkoa kagera Fatma Mwassa akizungumza na madaktari bingwa ofisini kwake na kueleza hali ilivyo mikakakati ya mkoa waliyonayo kuhusu watu wenye matatizo ya moyo


Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, akizungumza na Mwananchi ofisini kwake amesema ujio wa kambi ya madaktari hao utapunguza gharama kwa wananchi wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya matibabu ya moyo ya kibingwa katika Hospitali ya Bugando na JKCI.

Bila kutaja idadi kamili, Mwassa amesema; "Shinikizo la damu lilikuwa likiongoza kwa idadi ya wagonjwa waliokuwa wakitibiwa katika hospitali hiyo mfano shinikizo la damu peke yake wagonjwa wa nje walikuwa asilimia 7.92  na wagonjwa wa ndani walikuwa 5.58 ya wagonjwa waliokuwa wanalazwa hospitali ya Bukoba,"

Mkazi wa Kata ya Nshambya Manispaa ya Bukoba mkoani humo, Anajoyce Ngilwa mbali na kushukuru Serikali kwa kuleta madaktari hao, amesema kupitia kambi hiyo wataweza kubaini changamoto za kiafya zinazowatesa.

Mwandishi: Zawad Paschal

Mhariri: Prosper Kwigize


Post a Comment

0 Comments