Zaidi ya miti milioni 1 yapandwa halmashauri ya Mji Kasulu

Halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma imepanda miti million moja na laki mbili katika kata kumi na tano kwa kipindi cha mwaka 2023, 2024 ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira

Akizungumza na Buha news afisa mazingira wa halmashauri hiyo Wambura Mwita amesema upandaji huo wa miti ni kufatia tamko la serikali lililo wataka kila halmashauri lipande miti millioni moja na laki tano na kwamba kufikia mwezi Mei 2024 watafikia malengo ya kitaifa.

Wilaya ya Kasulu ni miongoni mwa maeneo ambayo yanakabiriwa na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ukataji miti holela sambamba ufyekaji wa misitu kwa ajili ya kupata nishati ya kupikia hususani kuni na mkaa.

Inaelezwa kuwa takribani hekta 400,000,000 za misitu mkoani Kigoma ikiwemo za hifadhi za Taifa za makere kusini, pori la akiba la Moyowosi/Kigosi, bonde la Mto Malagarasi, mto Ruiche, na ramsa za Uvinza zimeharibiwa na shughuli za binadamu hali inayotajwa kusababisha madhara ya kimazingira ikiwemo joto kali linalotokana na ongezeko la hewa ukaa.

Katika kukabiliana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni moja ya vyanzo vya uharibifu wa mazingira, Afisa mazingira wa halmashauri ya Mji wa Kasulu Bw. Wambura Mwita amebainisha kuwa matumizi ya nishati  safi ya kupikia ya gesi ndiyo njia pekee ya  kusaidia kupunguza uharibifu huo.

Aidha bw. Wambura amesema lengo la serikali ni kuhakikisha kufikia mwaka 2030 wananchi wote wawe na uwezo wa kutumia nishati ya gesi ya kupikia kwa ajili ya kuepusha uharibifu wa mazingira na  unao pelekea hewa ukaa

Wafanya biashara ya mkaa wakiingia mjini Kasulu kutoka vijiji vyenye misitu ya asili ambayo iko hatarini kutoweka

Awali, Bw. Mahuna John ambaye ni mmiliki wa kitalu cha miti katika eneoo la Bongwe mjini Kasulu alieleza kuwa wamiliki wa misitu wilayani humo hawajanufaika na mpango wa kimataifa wa kudhibiti hewa ukaa ambao hutoa fedha kwa wenye mashamba ya miti

Bw. Mahuna amebainisha kuwa waoteshaji na wakulima wa miti wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa mitaji na kuiomba serikali kuweka vigezo na mashart rahisi ya upatikanaji wa fedha ajili ya kuzuia na kupambana na hewa ukaa

Ameeleza kuwa mbali na kuwa na jitihada kubwa katika kuthibiti hewa ukaa wanaomba serikali kuhimiza maafisa mazingira pamoja na misitu kuweka mikutano ya hadhara kwa ajili kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya gesi ya kupikia na kuachana na matumzi ya kuni na mkaa.

Mbunge wa Kasulu mjini Prof. Joyce Ndalichako akitoa mtundi wa gesi ulioambatana na jiko lake kwa Baba na Mama lishe mjini kasulu kama sehemu ya kuhimiza matumizi ya nishati mbadala ili kunusuru mazingira na kumtua kuni mama kichwani

Kwa upande wake Suleimani Tryphone ambaye ni mfanyabiashara wa chakula mjini Kasulu amekiri kuwepo kwa changamoto za kimazingira kwa jamii na kueleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia imemsaidia katika kurahisisha muda wakati wa uandaaji wa chakula pamoja na kujikinga na magonjwa yatokanayo na moshi wa kuni pamoja na mkaa

Amebainisha kuwa yapo madhara mengi yatokanayo na matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ikiwemo na uharibifu wa mazingira pamoja na matatizo ya kiafya kwa jamii hususani wanawake ambao kwa desturi ndio hujishughulisha na mapishi.

Jumla ya majiko ya gesi 900 yamegawiwa kwa wananchi katika Jimbo la Kasulu mjini chini ya uratibu wa mbunge wa jimbo hilo Prof. Joyce Ndalichako ambaye pia ni Waziri wa Nchi, ofisi ya waziri mkuu Kazi, ajira, vijana na wenye ulemavu.

Mwandishi: Sara Mataro

Mhariri: Adela Madyane

 


Post a Comment

0 Comments