Mafuriko katika bonde la Katubuka yaliyoanza mnamo mwezi Disemba mwaka 2023 yaliyosababisha zaidi ya watu 100 kuhama makazi yao na kufungwa kwa barabara kuu iendayo uwanja wa ndege wa mkoa wa Kigoma yameleta madhara zaidi kwa kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Akitoa taarifa ya kifo hicho, diwani wa kata ya Katubuka Moshi Mayengo amesema amepata taarifa hiyo majira ya saa nne asubuhi ya leo tarehe 14 Aprili 2024, kutoka kwa wasamaria walioona mwili wake ukielea juu ya maji.
Amesema kutokana na mwili huo kuharibika wameshindwa kuutambua na kuwaomba wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwaajili ya kuuhifadhi katika makaburi ya Masanga kwani haiwezekani kuendelea kuuhifadhi zaidi kutokana na uharibifu huo.
Askari wa jeshi la Zima moto na uokoaji wakielekea kwenye mtumbwi kwenda kuopoa mwili wa mtu aliyebainika kufariki dunia katika kipindi kisichojulikana ndani ya maji yaliyofurika katika kata ya Katubuka mjini Kigoma kwa zaidi ya mienzi mitano
Mwili wa mtu ambaye hajafahamika ukiwa juu ya machele paaba ya kuopolea majini katika barabara ya uwanja wa ndege mjini Kigoma
Diwani Mayengo ameiomba serikali kuituma kamati ya maafa kwaajili ya kutathmini uharibifu ununaoendelea kujitokeza katika eneo hilo kama wanavyofanya katika maeneo mengine ya nchi yaliyokumbwa na adha ya mafuriko, sambamba na kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuchukua tahadhari
Akizungumza inspekta Jacob Chacha kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto mkoani humo amewataka wananchi kusitisha shughuli zozote za kibinadamu zinazoendelea katika bonde hilo ambazo zinahusisha uvuvi wa samaki, wafanyabiashara kuosha mbogamboga pamoja na bodada kuosha pikipiki zao kwani ni hatari.
“Nawaomba wananchi kuacha mara moja kupita katika maji yaliyotuwama kwani ni hatari, hayo maji ni machafu kutokana na uwepo wa vyoo vya makazi ya watu yaliyozama, hayafai kwa matumizi yoyote ile hata ya uvuvi wa samaki, tuzingatie maelekezo tunayopewa na viongozi ili kuepuka vifo vinavyoweza kuepukika” Amesema inspekta Chacha.
Wakizungumza baadhi ya wananchi, Salum Nasoro muwekezaji wa nishati ya mafuta katika kampuni ya Salmo oil amewaomba wananchi kuhama katika maeneo hayo kwakuwa sasa ni hatarishi na kwamba hata yeye pamoja na uwekezaji mkubwa alioufanya ameamua kuhamisha malighafi zake mpaka pale maji hayo yatakapodhibitiwa.
Naye Baraka Kibutu mkazi wa Mangurueni ameimba serikali kutafuta namna ya kuondoa maji hayo kwani yanazidi kuleta madhara kwa wakazi wa eneo hilo ambapo nyumba zaidi zianzidi kuvamiwa na maji na kuanza kupasuka jambo linaloashiria hatari kwa familia zinazoishi ndani ya nyumba hizo.
0 Comments