Katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wananchi wilayani Muleba mkoani Kagera wamehimizwa kuendelea kudumisha mila, desturi, umoja na mshikamano kwa mustakabali wa nchi ya Tanzania.
Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga amesema hayo leo wakati wa ibada maalum ya kuliombea Taifa na viongozi sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Muleba .
Dkt Nyamahanga amesema kila mwananchi anatakiwa kuendelea kuuheshimu Muungano huo kwa kudumisha amani iliyopo kwani viongozi waliohasisi jambo hilo waliamini kuwa umoja ni Nguvu .
Amesema kuwa jambo lililofanywa na viongozi Katika kuchanganya udongo wa pande mbili tafsiri yake ilikuwa ni kuunganisha watanzania hivyo hakuna mtu atakayeweza kuwatenganisha kwa namna yoyote kila mmoja anatakiwa kuendelea kuuheshimu Muungano ili uweze kudumu .
Ameongeza kuwa Muungano huo ndo unawapa heshima watanzania,unawapa heshima ya uhuru Watanzania na unayapa hadhi mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwamba wote ni familia moja kwani ukienda Zanzibar unawakuta Watanzania wanafanya Biashara na ukija Tanzania unamkuta Mzanzibar anafanya biashara na hayo ndiyo mafanikio ya Muungano.
Shekhe Nurani Amri akiomba wakati wa ibada maalum ya kuliombea Taifa,Viongozi wa Kitaifa ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya MuunganoKwa upande wao baadhi ya viongozi walioongoza ibada hiyo Shekhe Nurani Amri pamoja na Mwinjilisiti kutoka kanisa la Kiinjiri la Kirutheri Tanzania wilaya ya Muleba Felician Mathias wamewahimiza Watanzania kuendelea kuwaombea viongozi waliopo madarakani wakati wote wanapopata nafasi ya kuomba ili waweze kuendelea kuwaongoza katika misingi inayompendeza mwenyezi Mungu.
Kabla ya ibada hiyo viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Muleba , Watumishi pamoja na wananchi wa wilaya hiyo waliungana kwa pamoja kufanya usafi katika kituo cha afya Kaigara kilichopo wilayani humo ambapo kesho watashiriki katika michezo mbalimbali.
Mwandishi: Mariam Kagenda
Mhariri: Prosper Kwigize
0 Comments