Mkuu wa wilaya Kasulu atoa maagizo kwa watumishi wa idara ya Afya

Mkuu wa wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma Kanali Issack Mwakisu amewataka watumishi viongozi wa kada za afya katika halmashauri ya mji na vijijini kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maadili ya taaluma na utumishi wa umma pamoja na huduma bora kwa wagonjwa.

Agizo hilo ameliotoja jana katika kikao kazi cha watumishi viongozi wa kada za afya kilicho fanyika katika ukumbi mdogo wa ofisi ya mkuu wa wilaya mjini Kasulu akibainisha kuwepo kwa baadhi ya watumishi wasiozingatia maadili ya Kazi zao.

Ameeleza kuwa baaadhi ya watumishi katika vituo vya afya wamekuwa wakifanya kazi pasipo kufata misingi ya taaluma ya kazi yao pamoja na kutoa lugha chafu kwa wagonjwa hali inayo pelekea wagonjwa wengi kukata tamaa na kukosa matumaini.

Amefafanua kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi juu ya watumishi wa afya ikiwemo kutotunza siri za mgonjwa na muuguzi kitendo kinacho shusha ubora na ufanisi wa utendaji kazi wa vituo vya afya.

Kufuatia hali hiyo Kanali Mwakisu amewataka watumishi wote wa afya kuanzia ngazi ya kijiji, kata na hospitali ya wilaya kuanzia April 20, 2024 kufanya usafi wa kila kituo na kutoa taarifa na picha kuhusu shughuli zinazo endelea kama uzinduzi wa kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Awali akiwasilisha ripoti yake, afisa wa afya kutoka hospitali ya Mji wa Kasulu Mlimani Bw. Malimi Ntemiseni amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassani kupitia kwa mkuu wa wilaya ya kasulu kwa kazi nzuri anayofanya hususani kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya afya ikiwemo kukarabati baadhi ya miundo mbinu ya hospitali kama maji na umeme na kuongeza vifaa wezeshi.

Sambamba na shukrani hizo Bw. Ntemiseni ameleza baadhi ya changamoto mbali mbali za hospitali na mazingira zinazo wakwamisha wauguuzi kutekeleza wajibu wao kuwa ni kutokuwepo na waajiriwa rasmi wa kada ya usafi wa mazingira kunakosababisha wauguzi kutumia mda wa kuhudumia wagonjwa kufanya usafi.

Kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtewele amehimiza watumishi kutekeleza misingi na wajibu wa watumishi wa sekta afya akibainisha baadhi ya haki na wajibu kwa mtumishi wa umma kuwa ni kulipwa mshahara baada ya kutekeleza wajibu.

Ameeleza kuwa mtumishi wa umma anao wajibu wa kuchangia na kuongeza ubora wa huduma za hospitali kwa kuwa mbunifu wa mambo mbali mbali kama kuboresha miundo mbinu ya hospitali na kupeleka mapendekezo yake kwa mkurugenzi kwa lengo la kutendewa kazi.

Wakati huo huo Serikali wilayani Kasulu imekemea kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika maeneo ya kutolea huduma ikiwemo kuuzwa kwa kadi za kliniki kwa mama wenye ujauzito pamoja na watoto.

  

Post a Comment

0 Comments