Wahitimu wa mafunzo ya Ualimu katika chuo cha Ualimu Katoke Daraja A kilichopo wilayani Muleba mkoani Kagera wamehimizwa kuomba nafasi za kujitolea katika maeneo yao wakati wakisubiri ajira na kutokukubali kukaa nyumbani bila kuwa na kazi yoyote ya kufanya .
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatuma Mwassa amesema hayo wakati wa Maafali ya 85 ya chuo cha ualimu katoke kwa wanafunzi wa mafunzo ya ualimu daraja A yaliyofanyika chuoni hapo April 25.
Mh Mwassa amesema kuwa mkoa huo utatoa fursa za kujitolea kwa wanafunzi waliohitimu mafunzo ya Ualimu kujitolea kufundisha katika shule zilizopo mkoa wa Kagera hivyo wanafunzi hao hawatakiwi kukaa nyumbani kuosha vyombo na kusaidia kupika badala yake wajishughulishe katika shughuli mbalimbali
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatuma Mwassa wakati akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya Ualimu daraja A chuo cha Ualimu Katoke
Amesema kuwa kwa wale ambao hawatokuwa kwenye fursa za kujitolea wanaweza kufungua biashara ndogo ndogo za Mpesa na ujasiriamali kwani wakati wako chuoni wamefundishwa ni kwa jinsi gani wanaweza kujikwamua kiuchumi ili waweze kuingiza kipato hata kidogo badala ya kutegemea wazaziKwa upande wake mkuu wa chuo hicho Bwana Michael Ntwale ameiomba serikali kuwatatulia changamoto ya ukosefu wa nishati mbadala amesema kuwa licha ya kuwa ukatikaji wa umeme kutokuwa wa mara kwa mara kama ilivyokuwa awali lakini wakiwa na nishati mbadala itawasaidia wanafunzi wa chuo hicho inapotokea umeme ukakatika .
Naye Emmanuel Jonas wakati akisoma Risala kwa niaba ya wahitimu hao amesema kuwa walianza masomo yao mwaka 2022 wakiwa wanafunzi 202 lakini waliohitimu ni 198 na wengine 4 waliondoka chuoni kutokana na sababu mbalimbali.
Aidha amesema kuwa licha ya mafanikio zipo changamoto mbalimbali ambazo wangeomba serikali kuzitatua ikiwa ni pamoja na ukosefu wa nishati mbadala kwa ajili ya kujisomea pindi umeme unapokatika, uchakavu wa nyumba na makazi wanayoishi watumishi wa chuo pamoja na uchakavu wa mashine ya kusambaza maji kwenye chuo hicho.
0 Comments