Prof. Ndalichako akabidhi gari la wagonjwa Nyansha Kasulu

 

Mbunge wa Jimbo la Kasulu mjini Profesa Joyce Ndalichako amekabidhi gari la wagonjwa lililotolewa na serikali kwa ajili ya kituo cha Afya Nyansha cha mjini Kasulu ili kurahisisha shughuli za utoaji wa huduma za afya na rufaa kwa wagonjwa

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi gari hilo leo katika kituo cha afya Nyansha kata ya Nyansha mjini Kasulu, Prof. Ndalishako ameishukuru serikali ya Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa gari hilo na kuwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

Amesisitiza kuwa serikali imekuwa sikivu kila anapopelekwa maombi na hoja za maendeleo katika jimbo hilo akibainisha kuwa pamoja na kutoa takribani magari matatu ya wagonjwa ndani ya jimbo katika kipindi kisichofika miezi sita, serikali imejenga vituo vipya vya afya viwili pamoja na zahanati mpya nane (8) mjini Kasulu

"Nilipokea kilio cha wananchi wa Nyansha kuhusu changamoto ya kusafirisha wagonjwa wanaopata rufaa kwenda kupata matibabu zaidi katika hospitali ya Mji na hospitali za rufaa, nikawasilisha kilio hicho kwa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na hatimaye amejibu maombi hayo" Amesisitiza Ndalichako

Profesa Joyce Ndalichako akihutubia wakazi wa kata ya Nyansha mjini Kasulu kabla ya kukabidhi gari la wagonjwa

Amesisitiza kuwa ataendelea kuwatumikia wananchi kwa weledi kwa kuhakikisha anawakilisha mahitaji ya wananchi Bungeni sambamba na kusimamia miradi ya maendeleo ndani ya jimbo, huku akibainisha kuwa mafanikio ni makubwa na shughuli zinaendelea.

"Mie huwa sisemi mengi katika mikutano yangu, vitendo vinaongea zaidi, tumetekeleza miradi mingi ikiwemo ujenzi wa shule mpya ya msingi Kilombero katika kata yenu ya Nyansha, Tumechimba kisima kipya cha maji cha Nyantare na maji hayo yatasambazwa kwa wananchi wote wa kata ya Nyansha na maeneo mengine" Amebainisha Prof. Ndalichako

Prof. Ndalichako akikata utepe kuashiria kuanza rasmi kwa matumizi ya gari la wagonjwa lililokabidhiwa kwa kituo cha afya Nyansha mjini Kasulu

Profesa Ndalichako ameeleza kuwa tayari Serikali imetoa kiasi cha Sh. milioni 700 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa utandikaji wa mabomba kutoka kisima cha Nyantare kwenda kwa wananchi, huku akitoa wito kwa kila mwananchi kuzingatia taratibu za maombi ya kuunganishiwa maji nyumbani.

Awali, akisoma taarifa ya makabidhiano ya gari la wagonjwa la kituo cha afya Nyansha, Mganga mkuu wa halmshauri ya Mji wa Kasulu Dkt. Peter Janga amempongeza mbunge huyo kwa namna anavyoshughulikia changamoto mbalimbali za idara ya afya ikiwemo huduma za rufaa kwa kuwezesha upatikanani wa magari na vifaa tiba.

"Tunakushukuru sana Mh. Mbunge wetu kwa juhudi zako za kufanikisha uwepo wa kituo hiki na kwa kupata chombo hiki cha usafiri kwa wagonjwa, gari hili linaongeza idadi ya magari ya wagonjwa kufika manne (4) na yamepangwa kufanya kazi katika vituo vya afya Mwami Ntare- Herujuu, Nyansha, Kiganamo na Hospitali ya Mji ya Mlimani Kasulu" Amesema Dkt. Njanga katika hotuba yake iliyosomwa na kaimu katibu wa afya

Profesa Joyce Ndalichako akifurahia ndani ya gari la wagonjwa alilokabishi baada ya kulifanyia majaribio kwa kuliendesha kwa umbali wa mita 100

Prof. Ndalichako akicheza kwata la wasanii kufurahia kukabidhiwa kwa gari la wagonjwa katika kituo cha Afya Nyansha


Muonekano wa kituo cha afya Nyansha kilichopo mjini Kasulu, ni miongoni mwa vituo vipya vya afya viwili vilivyojengwa katika kipindi cha 2020/2023 cha utekelezaji wa Ilani ya CCM 


Post a Comment

0 Comments